Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nchini Tanzaniaimeahidi kuangamiza vikundi vya uhalifu vilivyoibuka katika Kata ya Makulu, jijini Dodoma vinavyojiita Panya Karoa.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Jumanne Sagini alitoa ahadi hiyo bungeni leo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Tawfiq.
Mbunge huyo alisema kumezuka vikundi vya wahalifu katika kata hiyo na kutaka kufahamu mkakati wa serikali kuhakikisha haviendelei kufanya uhalifu katika maeneo mengine.
Sagini alisema kazi ya kupambana na vikundi hivyo imeanza na baadhi ya vijana wamekamatwa.
Awali, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Pangawe, Haji Amour Haji, Sagini alisema Jeshi la Polisi litaendelea na kazi ya kulinda maisha ya watu na mali zao kwa kufanya doria, kuendesha operesheni na misako ili kuwabaini na kuwakamata wahalifu.
“Jeshi la Polisi limewapanga wakaguzi wa polisi kila shehia katika Jimbo la Pangawe ili kusimamia usalama na kuishirikisha jamii kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi lipo imara kukabili vikundi vya uhalifu Zanzibar.
Wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya, Sagini alisema uhalifu ni zao la jamii hivyo akahimiza ushirikiano wa wazazi, walezi, viongozi wa dini na serikali kukabili vitendo hvyo ukiwamo ukatili kwa wanawake, wanaume, watoto na mauaji.