Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania imesema mwaka wa fedha 2022/2023, serikali ya nchi hiyo ina mpango wa kununua boti 320 za uvuvi kwa ajili ya kukopesha wavuvi wadogo na wa kati ili waboreshe kazi zao.
Waziri wa wizara hiyo, Mashimba Ndaki alisema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe, Jospeh Mkundi.
Mbunge huyo alisema wavuvi wengi wanakosa elimu, taarifa za kutosha kuhusu masoko na zana za kuongeza thamani ya wanachokivua, hivyo alitaka kufahamu mkakati wa serikali kuwasaidia wananchi hao.
Akijibu, Ndaki alisema serikali ina mpango mkakati wa kuwasaidia wavuvi ili waongeze tija na vipato na kwamba boti watakazokopeshwa zitawasaidia kuvua katika maji ya kina kirefu baharini na katika maziwa.
“Lakini pia tuna mpango wa kuboresha mialo yetu yote na kuijenga katika maeneo mbalimbali, pamoja na kuboresha masoko madogo ya wavuvi wetu kwa kujenga vichanja ili mazao yanayotolewa baharini au ziwani yapate mahali pa kuanikwa vizuri,” alisema.
Awali, Ndaki alisema katika uchumi unaozingatia misingi ya sera ya soko huria, ujenzi wa viwanda vikiwamo vya kuchakata samaki unafanywa na sekta binafsi.
Alisema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mkundi aliyetaka kufahamu serikali ina mkakati gani wa kuwezesha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki katika Wilaya ya Ukerewe.
“Jukumu la serikali ni kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na sekta nyingine za uzalishaji mali na utoaji huduma,” alisema Ndaki.
Alisema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kujenga viwanda vya kuchakata samaki katika Wilaya ya Ukerewe na maghala ya kuhifadhia na kugandisha mazao ya uvuvi.
Ndaki alisema serikali pia inaendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili pia kuwekeza kwenye maeneo ya ukanda mzima wa Ziwa Tanganyika kuanzia Kigoma kwenda Katavi hadi Rukwa.
Kuhusu minada, alisema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2022/2023, serikali imetenga Sh bilioni 21.2 kukarabati minada ya upili na ya mipakani.