Bunge la Somalia siku ya Jumamosi lilimuidhinisha kwa kauli moja Hamza Abdi Barre kama waziri mkuu mpya, na kufungua njia ya kuundwa kwa serikali mpya kwa ajili ya taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Wabunge wote 220 waliokuwepo walikubali uteuzi wa Barre, na kisha akaapishwa ofisini, spika wa bunge alisema.
Barre 48, aliliambia bunge kuwa ataunda serikali ambayo itazingatia “kuunda utulivu wa kisiasa unaojumuisha wote kulingana na kauli mbiu ya rais wa Somalia iliyopatanishwa ambayo iko katika amani na mataifa mengi.
Utawala mpya wa Somalia unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na njaa inayoambatana na uasi mkubwa wa kundi la wanajihadi la Al-Shabaab.
“Tutaunda serikali yenye uwezo ambayo inafuatilia vipaumbele vya taifa letu vya maendeleo na kibinadamu vinavyoangazia mahitaji ya watu wetu,” Barre aliandika kwenye Twitter.
Ukame mbaya katika eneo la Pembe ya Afrika umeacha takriban Wasomali milioni 7.1 — karibu nusu ya wakazi — wakipambana na njaa, huku zaidi ya 200,000 wakiwa kwenye ukingo wa njaa, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Al-Shabaab pia wanaendelea kufanya mashambulizi huku wakiwaua wanajeshi watatu katikati mwa Somalia, na kuweka wazi kazi ngumu inayowakabili viongozi wapya wa nchi hiyo.
Barre, mbunge kutoka jimbo linalojitawala la Jubaland alichaguliwa mapema mwezi huu na Rais Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alichaguliwa na bunge mwezi Mei baada ya mchakato wa upigaji kura uliochelewa kwa muda mrefu.
“Serikali yetu ina mpango kabambe wa sera ambao unalenga kuboresha usalama wetu, kuimarisha uchumi wetu na kutoa huduma za kimsingi kwa watu wetu,” Mohamud alisema kwenye Twitter baada ya Barre kuidhinishwa.
Kuna matumaini kwamba urais wa Mohamud utakomesha mzozo mkali wa kisiasa ambao uliharibu utawala wa mtangulizi wake Mohamed Abdullahi Mohamed, anayejulikana zaidi kama Farmajo, na kutishia kuirudisha nchi katika machafuko makali.
Barre anachukua nafasi ya Mohamed Hussein Roble, ambaye aliteuliwa mwaka wa 2020 na Farmajo lakini kisha akatofautiana na rais huyo wa zamani kuhusu kucheleweshwa kwa uchaguzi na masuala mengine ya kisiasa na usalama.
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia unaojulikana kama ATMIS ulitoa pongezi zake kwa Barre, kama alivyofanya Roble, ambaye alitoa wito kwa Wasomali wote kumuunga mkono mrithi wake.
Rais Mohamud mwenye umri wa miaka 66 hakufika kwenye kikao cha bunge baada ya kusema siku ya Ijumaa kwamba alipimwa na kukutwa na Covid-19.
Alitoa tangazo hilo kwenye Twitter baada ya kurejea kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, ikiwa ni safari yake ya kwanza rasmi nje ya nchi tangu kuchaguliwa kwake, akisema hana dalili zozote bali ataendelea kujitenga.
Mohamud ni mwanaharakati wa zamani wa elimu na amani ambaye hapo awali alikuwa rais kutoka 2012-2017 lakini ambaye utawala wake wa kwanza uligubikwa na madai ya ufisadi na mapigano.