ACHPR yaikosoa Tanzania kwa ukiukaji wa haki za binadamu kuelekea uchaguzi wa 2025

Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) imeitolea wito Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha inalinda, inaheshimu na inatekeleza kwa dhati viwango vya haki za binadamu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025.

Katika Azimio lake la hivi karibuni ACHPR/Res.640 (LXXXIV) 2025, lililotolewa wakati wa kikao chake cha 84 kilichofanyika kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 21 hadi 30 Julai 2025, Tume hiyo imeeleza “wasiwasi mkubwa” kuhusu kile ilichokitaja kuwa ni taarifa za ukiukaji wa haki za binadamu katika muktadha wa maandalizi ya uchaguzi huo mkuu.

Kuvunjwa kwa mikutano ya hadhara na kukamatwa kwa wapinzani

Tume hiyo imeonesha masikitiko yake juu ya ukandamizaji wa mikutano ya hadhara na mikusanyiko ya kisiasa, hususan matukio yaliyotokea tarehe 9 Aprili 2025, kufuatia kukamatwa kwa mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu, pamoja na tukio la 24 Aprili 2025, katika Mahakama ya Mwanzo Kisutu, ambako wafuasi wa upinzani walizuiwa kuhudhuria kesi ya Lissu.

Vilevile, Tume hiyo imeeleza wasiwasi wake kuhusu madai ya kutoweka kwa watu, mateso, na ukamatwaji holela, mambo ambayo pia yamelaaniwa na watetezi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa na taasisi kama Bunge la Ulaya.

Wasiwasi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii

Azimio hilo pia limeelezea hali ya sintofahamu kuhusu kukandamizwa kwa uhuru wa kujieleza na kupatikana kwa habari nchini Tanzania. ACHPR imekosoa hatua ya kuzuiwa kwa jukwaa la kijamii X (zamani Twitter) mnamo 4 Juni 2025, pamoja na kuwepo kwa vikwazo dhidi ya majukwaa mengine kama YouTube, Telegram, na Clubhouse, ambavyo vinapatikana tu kwa kutumia VPNs.

Kwa mujibu wa Tume hiyo, vizuizi hivyo vinakiuka haki ya wananchi kupata taarifa, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina

ACHPR imetoa mwito kwa Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi huru na wa kina kuhusu:

Madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kutoweka kwa watu, mateso na ukamataji holela, Vizuizi dhidi ya mikutano ya hadhara na mikusanyiko ya kisiasa, Utesaji na kuzuiwa kwa watetezi wa haki za binadamu kutoka Kenya na Uganda, waliodaiwa kuwekwa rumande na kisha kufukuzwa nchini mnamo Mei 2025 bila kufikishwa mahakamani.
Kufukuzwa kwa maafisa wa sheria wa kigeni

Azimio hilo pia limelaani hatua ya kuondolewa nchini kwa aliyekuwa Waziri wa Sheria na Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya, pamoja na timu yake, tarehe 18 Mei 2025, ambao walikuwa nchini kwa shughuli za haki za binadamu. Tukio hilo lilifuatwa siku moja baadaye na kufukuzwa kwa wanaharakati kutoka Kenya na Uganda. Tume hiyo inasema hakuna ushahidi kuwa hatua hizo zilizingatia mchakato wa kisheria au haki ya kujitetea.

Wito kwa uchaguzi huru na wa haki

Tume ya Afrika inaitaka Serikali ya Tanzania kuandaa mazingira wezeshi ya kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki, na wa amani. Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni:

Mosi, Kuhakikisha upatikanaji wa taarifa kwa uhuru, ikijumuisha mtandao usiofungwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi


Pili, Kulinda haki ya uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari;

Tatu, Kutoa ulinzi kwa watetezi wa haki za binadamu;

Nne, Kuwezesha wagombea binafsi kushiriki uchaguzi kwa mujibu wa amri ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu;


Tano, Kufanikisha mabadiliko ya kikatiba na kisheria kuhakikisha kuwa mahakama za ndani zina uwezo wa kuamua migogoro ya uchaguzi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African Charter), unaozitaka serikali kulinda na kuheshimu haki za binadamu. Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, Tanzania imekuwa chini ya uangalizi wa taasisi za haki za binadamu kutokana na baadhi ya hatua zinazoibua maswali kuhusu usawa wa kisiasa.

Tume ya Afrika, kupitia azimio hili, inatoa tahadhari kwamba mwenendo wa mambo kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025 unaweza kuathiri taswira ya Tanzania kimataifa ikiwa haki na uhuru wa kisiasa havitalindwa ipasavyo.