Chama cha ACT Wazalendo kimesema kinapinga vikali na kukemea kwa nguvu zote kauli za CCM na Mashabiki zake za kutaka kufungwa kwa mtandao wa X (zamani Twitter) ambapo ACT imesema ni wazi kuwa kauli hizo ni njama za Serikali katika mwendelezo wa kuzuia haki ya kupata taarifa na uhuru wa kutoa maoni kupitia majukwaa mbalimbali ya habari.
Akiongea Jijini Dar es salaam leo June 12,2024, Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa ACT Wazalendo, Rahma Mwita amesema Serikali ya CCM imekuwa na utamaduni wa kutovumilia maoni, mitazamo na fikra tofauti zinazotolewa na Wananchi kuhusu Viongozi na sera zao, na mara zote inatumia hila za namna tofautitofauti ili kutimiza dhamira hiyo kandamizi.
Itakumbukwa Juni 11,2024 Mohamed Kawaida, Mwenyekiti wa UVCCM aliitisha mkutano na wanahabari na kutoa tamko la kuishinikiza Serikali kufungia mtandao huo kwa madai kuwa unahamasisha ngono.
“Hivi karibuni tumepokea taarifa ambayo kidogo Vijana wa CCM imetushtua kidogo kupitia mtandao wetu huu ambao unaitwa mtandao wa X(Twitter) na sisi wengine tulishtuka mapema, kwanza ukitazama tu jina lake lenyewe limeshaanza kuitwa X maana yake Saikolojikali tumeaanza kuandaliwa ili kila kitu kinachokuja ndani yake tuone nicha kawaida sasa ndugu zetu hawa wametoa tangazo la kuruhusu kwamba maudhui yote ya kingono na mengineyo ambayo ukifuatilia tamaduni zetu kama Watanzania unaona ni vitu ambavyo hatuendani navyo, na tumeona kupitia Serikali yetu pendwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mitandao yote yenye maudhui ya namna hii wameifungia, sasa umefika wakati, Serikali yetu na mtandao huu kuufungia”- Mohamed Kawaida, Mwenyekiti wa UVCCM.
Hatua hii imehusishwa na nia ovu ya Serikali kutaka kutekeleza jambo hilo wakati huu ambapo Tanzania inajiandaa na Uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.
Chama cha ACT Wazalendo kimesema Serikali ina nia ya kutaka kuzima maoni huru ya wananchi dhidi ya watawala.
“Mbinu hizo zinaanza na sheria kandamizi kama vile Sheria ya Magazeti ya 1976, Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta 2010, Sheria za Makosa ya Kimtandao 2015, Sheria ya Takwimu 2015 na nyingine nyingi, Watanzania wamekuwa wakipitia mazingira magumu kutokana na hila za Serikali kudhibiti uhuru na maoni yao dhidi ya Watawala.Serikali imekuwa ikitoa mashambulizi kwa Wananchi kwa sura mbalimbali, wapo wanaotishwa, kutozwa fidia na kufungwa jela kwa kutoa maoni tofauti ambayo Serikali inayaita ‘makosa ya uchochezi’, vilevile tunashuhudia kufungiwa na kufutwa kwa vyombo vya habari, alimradi kuvifanya visifanye majukumu yao kwa uhuru”
Aidha wameitaka Serikali kutumia sheria zilizotungwa kudhibiti wanaotumia mitandao kuhamasisha ngono na sio kuifungia
“Hoja za maadili zinazotolewa na wapambe ni dhaifu, makosa ya maadili yamewekewa sheria na utaratibu wa kushughulikiwa, kama kuna Wananchi wanafanya makosa yoyote ya kimaadili mtandaoni (Twitter) zipo sheria sio kufunga mitandao, Serikali iache kujificha kwenye kichaka cha maadili, ACT Wazalendo inaungana na watanzania waliojitokeza kupinga chokochoko za Wapambe na baadhi ya Viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii, tunatoa wito kwa Wadau wote kushikamana ili kulinda uhuru wa kupata habari Nchini kwa kupinga hila zozote za Serikali kukandamiza haki hiyo”
Wakati ACT Wazalendo wakitoa kauli hiyo tayari baadhi ya viongozi wa dini wameunga mkono hoja hiyo ya UVCCM