ACT WAZALENDO WAMTAKA IGP SIRRO AJIUZULU

 IGP Simon Sirro 

Chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania, kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo IGP Simon Sirro kujiuzulu, kwa kile walichodai kuwa IGP huyo hana sifa ya kuliongoza jeshi hilo.Chama hicho cha upinzani kinachongozwa na mwanasiasa Zitto Kabwe, kimesema matamshi ya IGP Sirro ni kielelezo cha kukosa weledi na ni jambo la kusikitisha kwa mtu kama IGP kuwa na hulka ya jinai ni suala la mtu binafsi na si suala la familia ya mtu.

Agosti 27 IGP Simon Sirro akiwa katika viwanja vya Polisi Kurasini jijini Dar salaam, wakati wa kuaga miili ya askari waliouawa kwa kupigwa risasi na Hamza Mohamed(30), katika shambulio lililotokea makutano ya Barabara ya Kinondoni na Kenyatta Drive, Sirro aliwataka askari kuongeza umakini wanapokuwa na silaha na hawatakiwi kumwamini mtu kwa kuwa sio watu wote wanawapenda.

“Huwa na waambia siku zote, usicheze na mtu ovyo ovyo, usimuamini kila mtu, hii yote ni kwasababu ya imani. Walipomuona huyu Hamza walijua ni Mtanzania wa kawaida, kumbe alikuwa na silaha akawashambulia. Sisi askari tumeapa kufa kwa ajili ya kuwalinda Watanzania, lakini lazima Watanzania wajue na sisi tuna familia zetu,” IGP Sirro.

Kufuatia kauli hiyo watu mbalimbali mitandaoni waliiokosoa kauli hiyo na kusema kwamba kama IGP hakupaswa kusema hivyo.


Agosti 28, 2021 IGP Simon Sirro akiwa kwenye hafla ya kuwaaga makamishina wake waliostaafu, Sirro alitoa kauli ambayo wanaharakati wanasema imeutweza utu wa mtu na kuingilia haki zake binafsi.“Hiyo familia ya Hamza inajisikiaje, fikiria wewe ungekuwa baba yake Hamza, mama yake Hamza, mdogo wake ungejisikiaje kuzaa kwako umetuletea balaa Watanzania, kwahiyo naomba Watanzania wengine wasituzalie watoto kama Hamza” alisema IGP Sirro.

ACT Wazalendo

ACT Wazalendo wanasema matamshi haya si ya kiungwana kwani yanakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokataza adhabu za jumla, na ikizingatiwa kwamba Hamza ni mtu mzima aliyevuka umri wa miaka 18 hivyo anawajibika kwa matendo yake na si wazazi wake au ndugu zake.