ACT Wazalendo yalaani kukamatwa kwa M/kiti wa NETO, yataka aachiwe huru

Chama cha ACT Wazalendo kimelaani vikali kukamatwa kwa ndugu Joseph Paulo Kaheza, Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO), ambaye anashikiliwa na polisi mkoani Geita tangu jana Februari 24, 2025 

Kukamatwa kwake kunafuatia tamko la NETO la Februari 21, 2025 lililotaka serikali ichukue hatua madhubuti kukabiliana na tatizo la ajira kwa walimu waliomaliza masomo yao.

NETO, kupitia tamko lake, ilibainisha hila zinazotumiwa kuficha uhaba wa walimu, zikiwemo mfumo wa walimu wa kujitolea, changamoto za utaratibu mpya wa ajira za ualimu kupitia usaili na idadi ndogo ya nafasi za ajira zinazotolewa na serikali.

Taarifa iliyotolewa leo na Waziri Kivuli wa Sera, Bunge, Vijana, Kazi, na Ajira ndugu Ndolezi Petro wa ACT Wazalendo, imeeleza kusikitishwa kuona serikali badala kushugulikia madai yao, wanawatumia Polisi kuzima sauti za vijana hao. 

“Tatizo la ajira nchini Tanzania ni bomu linalotengenezwa na Serikali yenyewe, haliwezi kutatuliwa kwa propaganda, hila, vitisho, au kamata kamata ya vijana wanaohoji hali hii. Jeshi la Polisi haliwezi kutoa majibu ya ukosefu wa ajira, litasababisha machafukotu” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ina upungufu wa walimu 279,202 kwa shule za msingi na sekondari, huku vijana takribani 146,000 waliomaliza masomo ya ualimu wakikosa ajira na kuendelea kuzunguka mitaani. Upungufu huu wa walimu umeathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu na kuwabebesha walimu waliopo mzigo mkubwa wa kazi.

ACT Wazalendo wanaitaka serikali imuachie huru mara moja na bila masharti yoyote ndugu Joseph Paulo Kaheza na iache nia ya kuwakamata viongozi wengine, badala yake iongezwe bajeti ya serikali kuanzania mwaka wa fedha 2025/26 kutoa ajira takribani 65,000 kila mwaka kutatua tatizo la uhaba wa walimu shuleni na kuhakikisha ajira kwa vijana hao.

Pamoja na hayo imeahidi kusimama na walimu hao katika kupigania haki yao ya ajira na kupinga mfumo kandamizi unaozidi kuwanyima fursa.