ACT Wazalendo yaja na hoja sita kabla ya Uchaguzi Mkuu

Chama cha ACT Wazalendo kimeainisha mambo  sita ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi na Serikali na Tume ya Uchaguzi ambapo iwapo yatatekelezwa kwa vitendo yatajenga msingi wa kuaminiana miongoni mwa wadau wa uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Hoja hizo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi huru na haki wakati huu ambapo Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2025

Akizungumza katika Kongamano la Tatu la Operesheni Linda Demokrasia lililofanyika Mkoani Kigoma katika Jimbo la Kigoma Mjini jana  tarehe 6 Aprili 2025, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara Ndugu Isihaka Mchinjita amesema kuwa baadhi ya masuala hayo hayahitaji mabadiliko ya sheria bali ni usimamizi wa sheria zilizopo.

Akiainisha masuala hayo amesema,Suala la kwanza, kwa mujibu wa Ndugu Mchinjita ni kuhakikisha kuwa wajumbe wa sasa wa Tume Huru ya Uchaguzi wanaondolewa na wajumbe wapya wanateuliwa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa kwenye Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ikiwemo kutangaza nafasi hizo na kufanya usaili kwa Watanzania wenye sifa kupewa nafasi ya kuwa Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Pili, alisema Mchinjita, ni lazima vyombo vya ulinzi na usalama vijiondoshe katika kushiriki katika hujuma za kupora uchaguzi. Uzoefu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020 na Uchaguzi Wa Serikali za Mitaa 2024 umeonesha kuwa vyombo vya dola ikiwemo Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa vimejiingiza katika wizi kubariki na kushiriki katika vitendo vya wizi wa kura.

Tatu, ACT Wazalendo imesisitiza juu ya Wakurugenzi wa Halmashauri kutokuwa wasimamizi wa Uchaguzi. Kadhalika imeweka bayana kuwa Tume ya Uchaguzi inapaswa kuhakikisha kuwa mchakato unaoendelea sasa wa uteuzi wa wasimamizi na wasimamizi wa uchaguzi hauwahusishi Wakurugenzi wa Halmashauri ambao takribani wote ni makada wa Chama cha Mapinduzi.

Nne, hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha kuwa kura feki zinadhibitiwa kwenye mchakato wa uchaguzi. Mchinjita ameweka bayana kuwa ni lazima kuwa na uwazi na ushirikishaji kwenye mchakato mzima wa uzalishaji, usambazaji na udhibiti wa karatasi za kupigia kura.

Tano, mawakala ni lazima wawe huru katika vituo vya kupigia kura. Mchakato mzima wa upatikanaji, uapishaji na uwepo wa mawakala katika vituo vya kupigia kura ni lazima uzingatie maslahi mapana ya wagombea ikiwemo mawakala kupatiwa nakala za matokeo. Pia iwe ni mwiko kwa mawakala kuondolewa kwenye vituo vya kupigia kura.

Sita, kusiwe na kuenguliwa kwa wagombea. Tume ya Uchaguzi iweke utaratibu wa kurekebishwa kwa makosa ya kiuandishi katika fomu za wagombea badala ya kuendelea kuwaengua wagombea wa upinzani pekee.

Kwa upande wa Zanzibar, masuala ya kipaumbele yametajwa kuwa ni kuondolewa kwa kura ya mapema, kuondolewa kwa Mkurugenzi wa ZEC na Sekretarieti yake na uandikishaji wa wapigakura bila ubaguzi.

Ndugu Mchinjita ameweka bayana kuwa hoja hizi zitawasilishwa majadiliano yanayoendelea kupitia Kituo cha Demokrasia (TCD). 

Katika hatua nyingine, Mchinjita ameweka bayana msimamo wa Chama hicho wa kutaka Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ufutwe na ufanywe sambamba na Uchaguzi Mkuu 2025.

Ndugu Mchinjita ameweka bayana kuwa Operesheni Linda Demokrasia ina lengo la kurejesha thamani ya kura ya kila Mtanzania na kwamba ACT Wazalendo inaendelea kuwahamasisha wananchi kuwa tayari kupigania thamani ya kura.

Chama cha ACT Wazalendo kinaendelea na Makongamano ya viongozi wa ngazi za chini kufafanua msimamo wa Chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025. Kongamano la Mkoa wa Kigoma ni la Tatu likitanguliwa na Makongamano ya Mikoa ya Dar es salaam na Lindi. Baada ya Kigoma, ACT Wazalendo kinatarajiwa kufanya Kongamano la Nne katika Mkoa wa Songwe tarehe 12 Aprili 2025.