Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Lusikwi wilayani Sengerema nchini Tanzania, Nyanzila Shome (17) amefariki dunia akidaiwa kupigwa na mzazi wake Jephta Shome aliyekuwa akimtuhumu kufanya mapenzi wa mtoto wa jirani yake.
Mwanafunzi huyo amekumbwa na mauti hayo ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza mtihani wa kidato cha pili shuleni hapo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Maili Makori amesema wanawasaka wazazi wa mtoto huyo waliotoweka mara baada ya mauaji hayo.
Amesema tukio hili lilitokea Oktoba 30 majira ya usiku, ambapo baba wa mtoto (Jephta Shome) anayeelezwa kuwa na tetesi za mwanaye kutembea na mtoto wa jirani yake, alipofika nyumbani alianza kumushambulia mwanafunzi huyo kwa kipigo, hali iliyosababisha kifo cha mtoto huyo.
Makori amewataka watu waache tabia ya kujichukulia sheria mikoni kwa kuwa wanavunja Sheria kwa kusababisha mauwaji yasiyo ya lazima.
“Jeshi la Polisi liko kazini kuwasaka wazazi wake popote walipo na tutawakamata kisha kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Makori.
Baadhi ya wananchi wilayani Sengerema waliozungumza na Mwananchi, wameeleza kusikitishwa na tukio hilo, huku wakiomba vyombo vya Dola kuchukua hatua kali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema, Bunuru Shekidele amesema ndoto za maisha ya mwanafunzi huyo zimeishia ukingoni baada ya kupoteza maisha kwa kupigwa na mzazi wake kitendo ambacho kimeleta simanzi kubwa miongoni mwa wananchi.
Shekidele amewataka wazazi kuwa makini wakati wa kuchukuwa maamuzi yoyote wanatakiwa kufanya uchunguzi juu ya tuhuma yoyote inayomuhusu mtu ndipo waweze kuchukuwa hatua.