Ado amshauri Nchemba kusimamia mchakato wa Katiba Mpya

Mbunge wa Tunduru Kaskazini kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, leo amesimama bungeni na kuunga mkono hoja ya uteuzi wa Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akitumia nafasi hiyo kuikumbusha serikali umuhimu wa kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kama sehemu ya maboresho ya demokrasia nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wachache wa upinzani waliopo bungeni Ado Shaibu alisema yeye na wenzake wachache wanaowakilisha upinzani bungeni hapo wameamua kuunga mkono uteuzi huo “kama ishara ya kumkopesha imani” Waziri Mkuu mpya, likiwa ni tamko adimu kutoka kwa upande wa upinzani katika mazingira ya kisiasa yaliyotawaliwa na chama tawala.

“Ni vigumu kusema kwa uhakika sifa zote zilizomfanya Mheshimiwa Rais kumteua Dkt. Mwigulu, lakini sifa moja nina uhakika nayo ni mtu mchapa kazi,” alisema Shaibu.

Aliongeza kuwa upinzani unatarajia Waziri Mkuu huyo mpya atasimamia kikamilifu rasilimali za taifa kwa manufaa ya wananchi na kuhakikisha serikali inafanya kazi kwa ufanisi, akisema:

“Kwetu sisi wachache, tunakuunga mkono kwa imani kwamba utachapa kazi. Tunatarajia utaongoza serikali yenye uwajibikaji na yenye kuwaletea Watanzania maendeleo.”

-Wito kuhusu demokrasia na Katiba Mpya-

Shaibu alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kusisitiza haja ya kuimarishwa kwa mfumo wa kidemokrasia na kurejesha ajenda ya Katiba Mpya, akisema kuwa Waziri Mkuu ana nafasi ya kipekee ya kuongoza mageuzi hayo kwa kuwa tasnia ya siasa na vyama vya siasa ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Tunaamini utaisimamia maboresho ya demokrasia nchini na kuipatia Tanzania Katiba Mpya, hasa ikizingatiwa kwamba siasa na vyama vya siasa viko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema.

Kauli hiyo imechukuliwa kama ujumbe mahsusi wa kisiasa kutoka upinzani kwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la kuhuisha mchakato wa Katiba ulioahirishwa tangu mwaka 2014.

Mbunge huyo wa ACT-Wazalendo pia alimhimiza Dkt. Nchemba kudumisha mtindo wake wa utendaji wa karibu na wananchi badala ya kubaki ofisini.

“Tuna imani hutakuwa Waziri Mkuu wa ofisini muda wote, bali Waziri Mkuu wa “field” kama ilivyokuwa desturi yako tulivyokuzoea,” alisema.

Uteuzi wa Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango, unakuja katika kipindi ambacho Tanzania inakabiliana na changamoto za kiuchumi na matarajio ya mageuzi ya kisiasa.

Vyama vya upinzani na wadau wa kiraia wamekuwa wakisisitiza kuwa serikali inapaswa kutumia kipindi hiki kuanzisha mazungumzo mapya ya kitaifa kuhusu Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi, na uwiano wa madaraka kati ya mihimili ya dola.