Afisa wa polisi amuua mpenzi wake, mke wa afisa mwenzake na kisha kujitoa uhai

Afisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Langata, jijini Nairobi amewaua kwa kuwapiga risasi wanawake wawili na kisha kujitoa uhai.
Kulingana na ripoti, Bwana Mark Mulanda alitanguliza kwa kumfyatulia risasi mke wa afisa mwenzake na kisha badaye kummiminia risasi mpenzi wake kabla ya kujitia kitanzi kwa kujipiga risasi kichwani.

Waliouawa na afisa huyo walitambuliwa kama Bi Fiona Chepkoech mwenye umri wa miaka 37, mkewe afisa wa polisi mwenzake na Rhoda Chepchumba ambaye alikuwa mpenzi wake.

Inadaiwa kuwa Mulanda aliondoka katika stesheni na kueleza wenzake anaelekea chumbani kwake kuchukua koti lake na alipofika kwa nyumba, ugomvi na mpenziwe ukaanza papo hapo. Ni hapo ambapo Fiona aliwasili kutaka kujua ni kipi kinachojiri na kwa bahati mbaya akakumbana na mauti baada ya Mulanda kummiminia risasi mara mbili na akaaga papo hapo.
Mulanda kisha akarejea chumbani na kumfyatulia Rhoda risasi saba na vile vile akafariki papo hapo. Kisha baadaye akajipiga risasi kichwani na pia kufariki. Tukio hilo lilifanyika Jumapili jioni, tarehe 5 mwezi Machi 2023.
Inasemeka watatu hao walikuwa wakiishi kakika nyumba za polisi zilizoko maeneo ya Mugumuini jijini Nairobi. Wakati wa tukio, mumewe Fiona anasemekana alikuwa ameondoka kwa muda kuelekea mashambani kwa shughuli za mazishi.
Afisa Mkuu wa polisi Kaunti ndogo ya Langata alifika kwenye eneo la tukio na kusema uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha mauaji hayo