Search
Close this search box.
Africa

Mkazi wa Kijiji cha Komarera wilayani Tarime mkoani Mara, Mwinga Kerambo, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia mama yake mzazi, Bhoke Mohere kwa kumniga shingo na kumnyonga hadi kufa.

Imedaiwa kuwa mama huyo aligoma kumpa kipande cha ardhi ya shamba, alichokuwa akitaka mtoto wake.

Akisomewa hukumu hiyo Mei 25, katika Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mahakama ya Wilaya Tarime chini ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Frank Moshi, Mwanasheria wa Serikali, Yese Temba, alidai mahakamani kuwa mshtakiwa Kerambo, Oktoba 19, 2019 akiwa nyumbani na mama yake alimlazimisha kumpa eneo la ardhi ya shamba na mama huyo aligoma kumpa.

Mwanasheria Temba alidai mshtakiwa Mwinga alichukua uamuzi wa kumshambulia mama yake kwa kumniga shingo na kumnyonga hadi kufa.

Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita vikiwamo vielelezo vya PF 3 na mganga aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu.

Mshtakiwa katika kesi hiyo alijitetea mwenyewe bila ya ushahidi mwingine wa kumuunga mkono.

Msajili wa Mhakama Kuu Moshi alisema kulingana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, mahakama haina pingamizi na shaka yoyote katika ushahidi huo.

“Mshtakiwa alimuua mama yake kwa makusudi, mahakama hii inakuhukumu kunyongwa hadi kufa ili iwe fundisho kwa watu wengine kama hao ambao hawana maadili mema hata kwa wazazi wao,” alisema Moshi.

Comments are closed