Ahukumiwa kunyongwa kwa kuwaua kwa kukusuidia walinzi wawili

Mahakama Kuu nchini Tanzania Kanda ya Dodoma, imemhukumu fundi ujenzi Maarufu January Haule (42) kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kukusudia la kuwaua kwa kutumia sululu walinzi wawili wa kituo cha kuuza mafuta cha state Oilcom kilichopo eneo la  Kisesa jijini Dodoma.

Katika kesi hiyo ya Jinai Namba  47 ya mwaka 2020, Haule alifanya tukio hilo Septemba 2015 kwa kuwapiga kichwani kwa kutumia sululu Paul Nduruma na Aloyce Patsango kwa madai walikuwa wakimnyanyasa katika shughuli zake za ujenzi.

Jaji Dk. Adam Mambi alisema siku ya tukio mshtakiwa alimaliza kazi zake na kuondoka na sululu ambayo aliificha katika shimo na ndio iliyotumika katika mauaji hayo.

Jaji alisema mshtakiwa alirudi eneo la tukio bila ya walinzi kujua na kusubiri muda wa saa sita usiku ambapo walinzi hao walikuwa wamelala ndipo alimpiga Nduruma kichwani mara mbili na baadae kumfuata Aloyce Patsango na kumpiga mara tatu kichwani.

Jaji Dk. Mambi alisema baada ya kutekeleza tukio hilo Haule alivunja kontena na kuiba mifuko ya saruji 60 aina ya twiga na kumpigia simu Mustapha Rajabu ambaye ni shahidi ili aweze kumuuzia kwa bei ya Sh. 10,000 kwa kila mfuko.

Hata hivyo Jaji Dk. Mambi alisema katika kesi za mauaji mara nyingi wanaangalia ushahidi wa mazingira kutokana na kwamba wauaji huwa wanajificha ili wasijulikane na kuongeza kuwa kitendo cha shahidi wa kwanza, watatu,wanne na watano kutoa ushahidi wao unaofanana moja kwa moja ushahidi wa mazingira unamtia hatiani mshtakiwa.

Pia mahakama iliangalia maoni ya wazee wa baraza ambapo ilijikita katika kuangalia hoja kama mshtakiwa anahusika katika mauaji hayo.

Jaji Dk. Mambi alisema baada ya ushahidi huo kukamilika mshtakiwa anahukumiwa kwa kifungu cha sheria cha 196 na 197 cha kanuni za adhabu ambapo mshtakiwa anapotenda kosa la kuuwa kwa kukusudia adhabu yake huwa ni moja kunyongwa hadi kufa.

Hata hivyo alisema mshtakiwa anaruhusiwa kukata rufaa kama hajaridhika na uamuzi wa mahakama.