Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Mara imemuhukumu kwenda jela miaka saba Msirari Muhere (60) mkazi wa Wilaya ya Tarime baada ya kupatikana na hatia ya kumuambukiza ugonjwa wa Ukimwi mtoto wa miaka sita kwa makusudi.
Hukumu hiyo imetolewa mjini hapa leo na Hakimu Mkazi Mkuu mwenye mamlaka ya ziada ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu, Timoth Swai baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.
Awali kesi hiyo ya jinai namba 7/2023 ilifunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime Juni 2021 na kutolewa hukumu Novemba 2022 ambapo hakimu wa mahakama hiyo ya Tarime aliamuru mshtakiwa huyo kulipa faini ya Sh200,000 au kwenda jela miaka mitano katika kesi hiyo iliyosajiliwa kwenye mahakama hiyo kwa namba 186/2021.
Kufuatia hukumu hiyo mshtakiwa huyo alilipa faini na kisha kuwa huru.
Hakimu Swai amesema kuwa kutokana na hukumu hiyo, Jamhuri ilikata rufaa Mahakama Kuu baada ya kutokuridhishwa na hukumu kwa maelezo ilikuwa kinyume cha Sheria ya Kuzuia Maambukizi ya Ukimwi namba 28 ya mwaka 2008.
“Sheria hii inatamka kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kusambaza Ukimwi kwa makusudi hukumu yake ni kifungo cha kati ya miaka mitano hadi 10 jela na hakuna chaguo la faini,”amesema.
Akitoa maelezo ya tukio hilo, hakimu Swai amesema kuwa mwaka 2018 Muhere alioa mke wa pili ambaye alikuwa na watoto watatu ambao aliamua kuishi nao pamoja na mama yao.
Amefafanua kuwa baadaye wanandoa hao waligombana hali iliyopelekea kutengana huku mwanamke huyo akiwaacha watoto wake watatu na baba yao huyo wa kufikia.
Ameongeza kuwa baadaye wanandoa hao walimaliza tofauti zao na kuanza kuishi tena pamoja kama mke na mume na kwamba baada ya muda mwanamke huyo aligundua kuwa mume wake aliwaambukiza watoto wake Ukimwi kwa makusudi.
“Ushahidi umeonyesha kuwa Muhere alichukua sindano na kunyonya damu kutoka kwa mtoto wa mke wake mkubwa ambaye alikuwa ameathirika kisha kuanza kuwadunga watoto wawili wa huyu mke wake wa pili na uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa kati ya hao watoto wawili mmoja wa kiume ameambukizwa ugonjwa wa Ukimwi,” amesema.
“Muhere na mke wake mkubwa ni waathirika wa Ukimwi na binti yao alizaliwa na ugonjwa huo kwa hiyo baada ya kutofautiana na mke mdogo aliamua kumkomesha kwa kuwaambukiza watoto wake Ukimwi labda kwasababu hawakuwa wa kwake (Muhere) wa kuzaa,” ameongeza.
Katika kesi ya awali jumla ya mashahidi sita walitoa ushahidi wao akiwemo mama pamoja na mtoto ambapo katika rufaa hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Felix Mshama na Joyce Matimbwi.