Ajali yaua watu watatu Tanga

Watu watatu wamefariki usiku wa kuamkia leo Ijumaa Januari 6,2023, baada ya lori lililokuwa limebeba gesi kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana eneo la ajali na kuthibitishwa na Polisi, zinasema ajali hiyo ilitokea saa 7.40 usiku, Januari 6, katika Kijiji cha Maili Kumi Wilaya ya Handeni katika barabara ya Segera.

Waliofariki kwa kuteketezwa na moto uliozuka kutokana na gesi kulipuka ni dereva wa lori la gesi na watu wawili ambao bado hajatambulika lakini walikuwa ndani ya Fuso iliyokuwa ikitokea Lushoto kwenda Dar es salaam.

Watu walioshudia tukio hilo wameieleza Mwananchi kuwa baada ya kugongana magari hayo ulilipuka moto na kusababisha eneo hilo kuwa na moto mkubwa ulioambatana na moshi.

“Ulilipuka moto mkubwa lori la gesi likaanza kuteketea na kusambaa, tukaanza kuwaokoa waliokuwemo ndani lakini tulishindwa,” amesema Makoroboi.

Amesema kutokana na moto huo barabara hiyo ikawa haipitiki na kusababisha foleni ya magari yaliyokuwa yakipita barabara hiyo.

Akizungumzia ajali hiyo leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Kamanda Henry Mwaibambe amesema baada ya tafrani hiyo, moto ulizimwa na barabara ikaanza kutumika kama kawaida.

“Majina ya waliokufa bado tunafuatilia tunatarajia kuyataja baada ya kuyapata, bado tunaendelea na uchunguzi,” amesema.

Chanzo:Mwananchi