Leo, Septemba 9,2024 mwili wa Ali Kibao, kada maarufu wa chama cha Chadema ambaye alifariki baada ya kutekwa umezikwa huku umati mkubwa wa watu umejitokeza kushuhudia safari yake ya mwisho iliyojaa huzuni ya kutafakarisha
Viongozi mbalimbali wa kisiasa na serikali wamefika kwenye msiba huo. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ambaye aliongozana na ujumbe wake kwenye hafla hiyo.
Hata hivyo vurugu zikaibuka mara tu alipowasili msibani hapo hata wakati wa hotuba yake kelele ziliongezeka zikimtaka Waziri Masauni kujiuzulu nafasi yake kutokana na matukio ya kutekwa wananchi yanayoendelea nchini huku Serikali haichukui hatua dhidi ya waharifu
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwatuliza wananchi hao na kuwaomba kumuacha Waziri Masauni kumaliza hotuba yake na alifanikiwa kumaliza hotuba hiyo.
Katika hotuba yake Masauni kuwa, watu hawapaswi kushutumu mtu kufuatia kifo cha aliyekuwa mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Ally Mohammed Kibao, na badala yake kama kuna mtu yeyote mwenye kielelezo kuhusu mauaji hayo awasilishe kwenye mamlaka husika.
“Nitoe wito kwa mtu yeyote kuacha kushutumu badala yake kama ana kielelezo cha mtu yeyote kuhusika na jambo hili akiwasilishe ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kusaidia kuweza kupata wahusika na waweze kuchukuliwa hatua,”
Aidha amesema Serikali imeanza kufatilia tukio hilo na kuihakikishia familia ya marehemu Ali Kibao pamoja na walioguswa na msiba huo kwamba itahakikisha waharifu wanakamatwa.
“Niwahakikishie waombolezaji wote hususan familia, kama Serikali hatutaliacha liende hivi hivi [mauaji ya Kibao], maelekezo ya Mheshimiwa Rais yameshaanza kutekelezwa, hatua zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika.”
-Mbowe asisitiza hofu ya usalama wa raia, ataka tume huru ya uchunguzi wa utekaji-
Kiongozi wa Chadema, Freeman Mbowe, alizungumza kwa hisia za huzuni na machungu, akieleza kwamba kifo cha Ali Kibao ni pigo kubwa kwa familia yake, chama, na taifa kwa ujumla. Mbowe alisisitiza kuwa kifo hiki kinatakiwa kuwa kichocheo cha kufanya mapitio makubwa katika usalama wa nchi na haki za kibinadamu. Alimtaja Kibao kama mfano wa ujasiri na dhamira katika kuleta mabadiliko nchini.
Amemtaka Waziri Masauni kuwasilisha rai ya waombolezaji kwa Rais Samia ya kuunda tume ya kijaji kuchunguza matukio yote ya aina hii kwani Rais ndiye mwenye mamlaka hiyo.
“Wote tumesikia kauli ya Rais ambayo inaelekeza vyombo vile vile ambavyo ndio watuhumiwa namba moja wakajichunguze wenyewe tunaona hilo haliwezekani, hii nchi haitarekebika”
“Tunaamini hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kusaidia ikaundwa tume ya kijaji ya kimahakama ikafanya uchunguzi wa jambo hili ili sisi wengine ambao inawezekana tuna baadhi ya Ushahidi ambao hatutakuwa tayari kuutoa polisi tutautoa kwa tume hii.
Itakumbukwa kuwa Kibao ambaye ni Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA, alitekwa mnamo Septemba 6,2024, eneo la Tegeta akiwa kwenye basi la Kampuni ya Tashirif linalofanya safari zake kutoka Dar es salaam kwenda Tanga, na watu walioshika silaa za moto wakijitambulisha kuwa ni askari, ambapo Septemba 8,2024 mwili wa Kibao ulionekana eneo la Ununio ukiwa na majeraha.
Matukio ya kutekwa na wasiojulikana nchini Tanzania yameshamiri huku watekaji wakiwa bado hawajatiwa mikononi mwa Polisi jambo linaloleta hofu kwa wananchi na kulifanya Jeshi la Polisi kuonekana halina weledi wa kufatilia matukio hayo.