Alicia Lissu: Mwaka mmoja bila mawasiliano na mumewe anayekabiliwa na kesi ya uhaini

Mke wa mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, Alicia Lissu, amesema hajazungumza wala kumuona mumewe kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu alipokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Alicia, ambaye kwa sasa anaishi nchini Ubelgiji, amesema amekuwa akifuatilia mwenendo wa kesi ya mumewe kupitia taarifa za mtandaoni, mawakili wake na ndugu wa familia.

Akizungumza na BBC Africa Eye, Alicia amesema miezi ya mwanzo baada ya kukamatwa kwa Lissu ilikuwa ya maumivu makubwa.

“Miezi mitatu ya kwanza ilikuwa migumu sana. Nilisongwa na mawazo,” amesema.

Tundu Lissu, mwenye umri wa miaka 58 na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alikamatwa mwezi Aprili 2025 alipokuwa akiendesha kampeni ya chama chake chini ya kaulimbiu ya “Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi.”

Mamlaka za Tanzania zilisema kampeni hiyo ilikuwa ikichochea wananchi kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, hali iliyosababisha kufunguliwa kwa kesi ya uhaini dhidi yake.

Alicia amesema alihofia usalama wa mumewe kutokana na uzito wa mashtaka hayo.

“Nilipatwa na hofu kubwa. Lissu alikuwa amekamatwa mara kadhaa hapo awali, lakini safari hii alikuwa anakabiliwa na shtaka kubwa zaidi,” amesema.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, shtaka la uhaini halina dhamana na linaweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo endapo mshtakiwa atapatikana na hatia. Alicia amesema kutokana na mazingira hayo, mawasiliano kati yake na mumewe yamekuwa ya nadra.

Kwa upande wake, Serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha madai kwamba uhuru wa kisiasa na nafasi ya kiraia vinazidi kubanwa nchini.

Katika maelezo iliyoyapa BBC mwezi Januari 2026, serikali ilisema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mazingira ya kisiasa yameendelea kufunguliwa kwa kuruhusu vyama vya siasa na wananchi kufanya mikutano na shughuli za kisiasa.

Serikali pia ilisema Tanzania imepiga hatua katika uhuru wa vyombo vya habari ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Kuhusu kesi ya Tundu Lissu, serikali ilisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba haiwezi kutoa maoni kuhusu shauri hilo kwa kuwa bado liko mahakamani. Aidha, ilieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kumkaribisha Lissu kurejea nchini kutoka uhamishoni ili kuendelea na shughuli zake za kisiasa.