Aliyegongwa na basi la mwendokasi atambuliwa na ndugu zake.

Majeruhi pekee wa ajali ya mwendokasi aliyekua amesalia Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ametambuliwa na ndugu zake akiwemo mkewe Isha Mohamed ambaye amekiri kumtafuta mumewe kwa siku 6.

Majeruhi huyo ayetambulika kwa jina la ‘Osam Milanzi’ na kutajwa kuwa mkazi wa Manzese Midizini, ametambuliwa siku moja baada ya kuanza kuongea na kujitaja kwa jina la Osam mkazi wa Manzese.

Taarifa iliyotolewa leo na Meneja Uhusiano wa (MOI), Patrick Mvungi imeeleza kuwa utambuzi umefanywa leo Februari 28, 2023 na mke wake Isha pamoja na mdogo wa Osam aitwaye Shaban Milanzi.

“Afya ya Osam imeimarika sana kutokana na kazi kubwa ambayo imefanywa na madaktari, wauguzi pamoja na watumishe wengine wa MOI.

“MOI tunatoa shukran za dhati kwa vyombo vya habari pamoja na Watanzania wote wenye mapenzi mema ambao washirikiana nasi kutangaza habari za kuwatafuta ndugu  wa Osam,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza kuwa Osam amehamishwa wodi ya wagonjwa mahututi na kupelekwa wodi ya kawaida.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12 asubuhi ikihusisha gari dogo ambalo dereva wake hakuzingatia sheria za barabarani kitendo kilichopelekea kugongwa na basi hilo. 

Mashuhuda wa ajali hiyo walisema dereva wa basi hilo alijitahidi kulikwepa gari dogo lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda kwani pamoja na kuligonga gari hilo aliishia kugonga ukuta wa jengo lililokuwepo upande wa kulia.

Katika ajali hiyo ambayo Osam alikuwa mtembea kwa miguu, Hospitali ya Taifa Muhimbili ilitoa taarifa kwamba imepokea majeruhi 37 na kwamba haijapokea kifo chochote

Video za CCTV Camera zilizosambaa mtandaoni Februari 22 zilimwonyesha Osam akitembea pembeni mwa barabara ya Kisutu kabla ya basi la mwendokasi halijamvamia na kumbamiza ukutani.