Aliyejifanya mkurugenzi wa usalama wa taifa ahukumiwa miaka mitano jela.

Mahakama ya Wilaya ya Iyonga Mlele, mkoani Katavi, imemuhukumu Raymond Bwire (28), kifungo cha miaka mitano jela, baada ya kukutwa na hatia ya kujifanya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mlele, Bilal Ahmed, alitoa hukumu hiyo Agosti 22 baada ya kesi namba 90 ya mwaka 2022 kusikilizwa mahakamani hapo na mshtakiwa kukutwa na hatia.

Kabla ya kusomwa hukumu hiyo, mwendesha mashtaka alidai kuwa Bwire ambaye ni mkazi wa Kamguluki Mkoa wa Mara, alikamatwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kutuma ujumbe mfupi kwenye simu ya mkononi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mlele, Theresia Irafy, akimtaka kumsaidia mdogo wake kupata kazi ya utendaji wa kijiji kwa kujitambulisha kwa jina la Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa Bwire alitenda kosa hilo Agosti 12, mwaka huu, mkoani Mara.