Search
Close this search box.
Africa

Mkurugenzi wa Mtandao wa Kijamii wa Uturn Collection, Allen Mhina (31),  na Mange Kimambi App, wameshtakiwa mahakamani kwa mashtaka matatu likiwamo la kuchapisha maudhui yanayokiuka haki na uhuru wa mtu mwingine.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanaamina Kombakono.

Miongoni mwa mashtaka mengine yanayowakabili ni kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kuwa na kibali kutoka bodi ya ithibati ya wanahabari na kumfedhesha mtu kwa njia ya mtandao.

Wakili Kombakono akisaidiana na Sylvia Mitanto, walidai kuwa Machi 9, 2022 katika maeneo tofauti ndani na nje ya Tanzania, washtakiwa walichapisha video ya aliyekuwa Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule, maarufu kama Profesa Jay, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) maudhui ambayo yanadhuru haki ya faragha ya mgonjwa (Profesa Jay).

 Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Septemba 22, 2021 na Machi 14, 2022, Kinondoni eneo la Manyanya  katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, mshtakiwa Allen na Kampuni ya Uturn Collection, walifanya kazi ya uandishi wa habari bila kuwa na kibali kutoka bodi ya ithibati ya wanahabari.

Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa Machi 9, 2022 katika maeneo tofauti ndani ya nje ya Tanzania, mshtakiwa Allen kupitia mfumo wa kompyuta unaojulikana kama Mange Kimambi APP, unaosimamiwa na Uturn Collection, alichapisha video ya aliyekuwa Profesa Jay ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa nia ya kusababisha hofu.

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi katika shauri hilo umekamilika na mshtakiwa Mhina anatarajiwa kusomewa maelezo ya awali Aprili 27, mwaka huu.

Hata hivyo, mtuhumiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya kudhaminiwa na mtu mmoja na kusaini bondi ya shilingi 100,000.

Comments are closed