Amnesty International yaitaka Tanzania kumwachilia huru kiongozi wa upinzani Tundu Lissu

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, limeitaka serikali ya Tanzania kumwachilia mara moja na bila masharti yoyote kiongozi wa chama cha upinzani Chadema, Tundu Lissu, aliyekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Lissu alikamatwa Jumatano akiwa pamoja na wanachama wengine wa Chadema baada ya kuhudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma, kusini mwa Tanzania. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, polisi walivamia mkutano huo na kuwatawanya wananchi kwa kutumia mabomu ya machozi.

Kesho yake, Alhamisi, Lissu alipelekwa katika mahakama jijini Dar es Salaam na kufunguliwa mashtaka ya uhaini — kosa ambalo linaweza kupewa adhabu ya kifo.

“Tunaitaka serikali ya Tanzania imwachilie Tundu Lissu mara moja na bila masharti yoyote,” alisema Tigere Chagutah, mkurugenzi wa kanda wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki na Kusini, katika taarifa yake siku ya Ijumaa jioni.

Chagutah alieleza kuwa serikali ya Tanzania imeendesha “kampeni ya ukandamizaji” dhidi ya wakosoaji wa serikali, na kwamba watu wanne waliokuwa wakosoaji wa serikali wamepotea kwa njia ya kutatanisha huku mmoja akiuawa kinyume cha sheria mwaka 2024.

Amesema pia kuwa polisi wamekuwa wakiwakamata wanachama wa upinzani kiholela, kuwazuilia bila msingi wa kisheria, pamoja na kutumia nguvu kupita kiasi katika kuwatawanya wafuasi wa vyama vya upinzani. Alikosoa vikali mbinu za mabavu zinazotumika kuwakandamiza wakosoaji wa serikali.

Chagutah ameitaka serikali ya Tanzania kulinda haki za msingi za binadamu, ikiwemo uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika kwa amani.

Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye awali alisifiwa kwa kuondoa baadhi ya masharti yaliyokuwa yamewekwa na mtangulizi wake John Magufuli dhidi ya vyama vya upinzani na vyombo vya habari, sasa anakosolewa vikali na makundi ya haki za binadamu pamoja na serikali za Magharibi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kurejea kwa mbinu za ukandamizaji.

Chama cha Chadema kimeishutumu serikali kwa kuendeleza vitisho dhidi ya viongozi na wafuasi wake, hali ambayo inaibua hofu kubwa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.