Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Amng’oa meno mkewe kisa shilingi 200 - Mwanzo TV

Amng’oa meno mkewe kisa shilingi 200

Jeshi la Polisi mkoani Mara linamshikilia mkazi mmoja wa Kijiji cha Nyakatende wilayani Musoma, Musa Abdallah kwa tuhuma za kumn’goa meno matatu mke wake kwa kutumia Praizi kwa kile kilichoelezwa ni ugomvi wa Sh. 200.

Inadaiwa mtuhumiwa huyo ambaye ni mganga wa kienyeji alitenda ukatili huo baada ya mke wake huyo kutumia fedha hizo, zilizotokana na mauzo ya mahindi kununua mahitaji ya mtoto wao mdogo bila idhini yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase, alithibitisha tukio hilo akisema mtuhumiwa huyo akisaidiana na mke wake mwingine ambaye bado hajatiwa nguvuni walimkamata mke mdogo wakamlaza chini na kisha mume wake akamn’goa meno matatu.

“Mtuhumiwa huyo akisaidiana na mke wake wa pili walimshika mama huyo na kumlaza chini huku wakiwa wamemshikilia ambapo kwa kutumia pliers aliweza kutenda ukatili huo na kumsababishia maumivu makali,” alisema.

Kamanda Morcase alisema hata hivyo, baada ya kutenda ukatili huo mtuhumiwa huyo ambaye yuko mikononi mwa polisi alimfungia ndani ya nyumba hadi taarifa kutoka wasamaria wema zilipofika polisi.

“Kwa sasa tunamshikilia kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi ili hatua sahihi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani kutokana na makosa yanayomkabili ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa polisi aliwatahadharisha wananchi kutumia njia sahihi za usuluhishi wakati wa migogoro, ikiwamo ya ndoa na kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa hatua hizo husababisha uvunjifu wa sheria.

Kwa mujibu wa baba mdogo wa mwathirika aliyefanyiwa ukatili huo, Emmanuel Mafuru, wawili hao wamekuwa katika ugomvi wa mara kwa mara katika ndoa yao siku za nyuma na jitihada za ndugu kuwasuluhisha hazikufua dafu.