Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro nchini Tanzania linamshikilia Msafiri Nasibu maarufu Mdede (31) kwa tuhuma za kumuua mkewe Mariam Vitalis (19) na mtoto wake Leila Msafiri (2).
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ijumaa, Agosti 12, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fotunatus Muslim, amesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya mauaji hayo jana usiku.
“Baada ya kufanya mauaji hayo mtuhumiwa alikwenda kwa kaka yake Salumu Nasibu na kumueleza kuwa amefanya mauaji na akamuaga kuwa anakimbia kijijini hapo,” amesema Musilimu.
Amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni migogoro ya kifamilia kati ya mtuhumiwa na marehemu mkewe.
Kwa upande wake diwani wa Kata Tegetelo, Yusuph Gomba amesema kuwa amepata taarifa za mauaji hayo leo asubuhi na alipofika eneo la tukio alikuta mtuhumiwa ameshakamatwa.