Amuua mtoto wake wa miaka mitatu kisha atoroka

ACP Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtafuta mzazi anayefahamika kwa jina la Daniel Muga, ambaye ni fundi ujenzi na mkazi wa Bombambili Ukonga Wilaya ya Ilala jiji humo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa miaka mitatu kwa kumpiga na kitu kizito kichwani.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP  Jumanne Muliro amesema tukio hilo lilitokea Februari 28, 2022 majira ya  saa 3:00 Usiku baada ya mzazi huyo kumpigia simu mke wake, Merry Joseph, ambaye walikuwa na mgogoro wa kifamilia na walikuwa wametengana kwa muda, huku muuwaji akidai alitaka aende alipokuwa ili ampe fedha za matumizi ya mtoto wao.

“Mama huyo akiwa na mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka mitatu alikubali wito huo na alipofika alibembelezwa ili warudiane lakini alikataa,” amesema Kamanda ACP Muliro.

Anaeleza kuwa wakati anaondoka ndipo alishambuliwa kwa kitu kizito kichwani yeye na mtoto wake hali iliyosababisha mtoto huyo kupoteza maisha na yeye kupata majeraha na kulazwa Hospitali ya Amana.

Kamande ACP Muliro amebainisha kuwa baada ya tukio hilo mtuhumiwa alitoroka.

Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo na kuwaomba wananchi wema kutoa taarifa kwenye kituo chochote cha Polisi au kwa mamlaka za kisheria zitakazowezesha mtuhumiwa huyo kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazomkabili.