Mkazi wa Kijiji cha Mahaha wilayani Magu mkoani Mwanza, Zawadi Msagaja (20) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hamo kwa tuhuma za kumzika mtoto wake akiwa hai ili apate mali.
Wengine wanaoshikiliwa katika tukio hilo ni dada yake Zawadi, Elizabeth Kaswa na mmewe, Mussa Mazuri ambaye ni mganga wa kienyeji aliyetoa maagizo ya kutekeleza kitendo hicho huku akimtishia Zawadi kuwa asipofanya hivyo yeye ndiyo atatolewa kafara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jana Novemba 29, 2022 ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema watuhumiwa wanadaiwa kutenda unyama huo Novemba 13 mwaka huu mchana katika mtaa wa Kisundi kata ya Bugogwa wilayani Ilemela mkoani humo.
“Zawadi ambaye ni mama wa mtoto alikuwa anaishi kwa dada yake kabla ya kuamriwa na shemeji yake ambaye ni mganga wa kienyeji kwamba amtoe kafara mtoto wake wa jinsia ya kike mwenye umri wa miezi miwili ili wapate utajiri,” amesema Mutafungwa
Amesema mwanamke huyo baada ya kukwepa kutolewa kafara aliridhia kumtoa mwanaye ambapo walimpatia mtoto huyo dawa za kienyeji zilizomfanya akose nguvu ilipofika Saa 2 usiku walimzika katika shamba lililopo wanapoishi akiwa hai.
Kamanda huyo amesema baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema, Polisi walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mama wa mtoto huyo na dada yake huku mganga huyo akikamatwa Novemba 21 mwaka huu katika kijiji cha Nyaguge wilayani Magu alikokuwa amejificha.
“Mwili wa mtoto ulipelekwa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kusubiri uchunguzi wa daktari. Upelelezi wa shauri hili unakamilishwa ili watuhumiwa wote wafikishiwe mahakamani,” amesema Kamanda Mtafungwa