Anayedaiwa kuiba Kishikwambi cha sensa kufikishwa mahakamani leo

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema mtuhumiwa anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi Tanzania,  baada ya kupora kishikwambi kwa karani wa sensa katika kata ya Majimoto halmashauri ya Mpimbwe atafikishwa mahakamani leo Augost 26, 2022.

Mwanamvua amebainisha hayo jana  Augost 25, 2022 wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake huku akisikitishwa na na kulaani kitendo hicho.

“Aliiba kishikwambi na mali zingine lakini alikamatwa, kesho mapema kizimabni hatuwezi kuvumilia watu wanaofanya uhalifu katika mkoa wetu,”

Amesema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa, kishikwambi hicho kilikaguliwa kilikuwa sawa hivyo kata ya Majimoto haikuathirika kuhesabiwa.

Amewataka makarani wote wa Sensa ya Watu na Makazi mkoani hapa kutumikia kiapo walichoapa, mafunzo na maelekezo ya Serikali.

“Wajibu na dhamana ya utunzaji wa vifaa vya sense ni wa kila karani kwasababu baada ya kumalizika tutamtaka aturejeshee vifanye kazi nyingine,”

“Wahakikishe wanalinda usalama wa vifaa mfano vishkwambi tayari zina taarifa za wananchi wetu kwahiyo haitakuwa vyema kusikia vimepotea au kuharibika,”amesema.

Hata hivyo amesema Sensa inaendelea vizuri hadi sasa kaya 56,363 zimehesabiwa huku akiwaonya wanaorusha picha za makarani mitandaoni.

“Unampiga picha karani wakati anatekeleza majukumu yake, nimeona kwenye mitandao ni kuvunja sheria na maadili atakayebainika atachukuliwa hatua,”amesema Mrindoko.