Shabani Awadhi (52), mkazi wa Igunga mkoani Tabora amefikishwa Mahakamani akituhumiwa kwa shambulio la aibu alilomtendea mtoto wa miaka tisa.
Mzee huyo anadaiwa kumvua nguo kisha kumwingizia kidole sehemu za siri binti wa darasa la pili mjini Igunga
Mwendesha Mashitaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Ellymajid Kweyamba ameiambia mahakama kuwa Machi 14 majira ya saa tano asubuhi katika Mtaa wa Kamando Kata ya Igunga Mjini, mshitakiwa alimshambulia mwanafunzi huyo kwa kumshika na kumvutia kwenye shamba la mahindi kisha kumvua nguo na kumwingizia kidole sehemu za siri kinyume na kifungu 138C(1)(a)(2)(b) kanuni ya adhabu sura 16 mapitio ya mwaka 2019.
Baada ya mshitakiwa kusomewa shitaka lake mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Igunga, Lydia Ilunda alikana kosa lakini mwendesha mashitaka akaiambia mahakama kuwa upelelezi umekamilika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 11 mshitakiwa atakapofikishwa mahakamani kusikiliza kesi yake hivyo kuendelea kubaki mahabusu.
Wakati huohuo, mkazi wa Mtaa wa Hanihani mjini Igunga, Christian Magesa (29) amepandishwa kizimbani akikabiliwa na tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi.
Akimsomea shitaka hilo, Kweyamba aliiambia mahakama kuwa Machi 20, saa saba na nusu usiku katika Mtaa wa Hanihani mjini hapa, mshitakiwa Christian Magesa alikamatwa na Mkaguzi wa Polisi Melchior Fundi akiwa na gramu 35 za bangi.
Mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo ambalo upelelezi wake umekamilika. Kesi imeahirishwa hadi Aprili 19 itakaposikilizwa na mshitakiwa yupo nje kwa dhamana ya shilingi 500,000 ya maneno.