Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya kikongwe mkazi wa kijiji cha Rigicha wilayani Serengeti, Wankuru Mwita (88) huku chanzo cha mauaji hayo kikidaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamamda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibushubwamu amesema kuwa watu hao wanatuhumiwa kumuua kwa kumkatakata kwa mapanga mwanamke huyo.
Miongoni mwa watuhumiwa wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo lililoteokea Januari 15 mwaka huu ni mke wa mtoto wa marehemu pamoja na waganga wawili wa kienyeji.
“Mmoja ni mke wa kijana wa marehemu na mume wake yupo jela anatumikia kifungo cha miaka 20 kwa kosa la ujangili sasa huyu binti ana watoto wanne ambao wamekuwa wakiugua ugua hivyo alikwenda kwa waganga wawili ambo wote walimwambia kuwa watoto hao wanalogwa na mama mkwe wake na anataka kuwaua “ amesema Kamanda Tibushubwamu
Amesema kuwa baada ya mke wa mtoto wa marehemu kuambiwa hivyo na waganga wote wawili, alikubaliana na mganga kufanya mpango wa kutafuta watu wa kumuua bibi huyo na kwamba bila bibi huyo kufa lazima angewauwa wajukuu zake.
“Mganga huyu ndiye aliyewatafuta hawa vijana watatu kisha kuwaosha na dawa kabla ya kwenda kuua na baada ya kuua walirudi tena kwake kuwaosha na dawa ili wasiweze kukamatwa na Polisi” amesema
Amesema kuwa kabla ya kufanya tukio hilo watuhumiwa hao walikubaliana kutekeleza jukumu hilo kwa malipo ya shilingi 500,000 wote kwa pamoja na kwamba walipewa shilingi 50,000 kama kianzio, pesa ambazo mama huyo alilipwa kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf) huku wakiahidiwa kumaliziwa kiasi cha shilingi 450,000.
Kamanda Tibushubwamu amesema kuwa watuhumiwa wote wamekiri kutenda kosa hilo na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.