Imeelezwa kuwa kiwango cha maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi ni watu 60,000 kila mwaka ambapo vijana wanaopata VVU maambukizi ni takribani asilimia 34.3 ya maambukizi mapya.
Haya yameelezwa leo Aprili 9,2025, bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo ameeleza kuwa takwimu zilizopo watu 1,690,948 wanaishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU).
“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo watu 1,690,948 wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU). Kadhalika, WAVIU 1,545,880 wanatumia dawa za kufubaza makali ya VVU ambapo watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni asilimia 96.4. 170”- amesema Waziri Mkuu.
Akisoma hotuba ya bajeti Waziri Majaliwa ametoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa UKIMWI bado ni tishio kama takwimu zinavyoonesha.
Amesema katika mwaka 2025/2026, Serikali itaendelea kuratibu shughuli za UKIMWI kwa kutoa huduma endelevu na stahimilivu kwa WAVIU; kuimarisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ili uweze kufanikisha malengo ya nchi katika kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030; kuweka msukumo katika kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika jamii ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Kadhalika amesema Serikali inatambua mabadiliko ya sera za misaada kutoka kwa baadhi ya wafadhili wetu wa muda mrefu wa masuala ya UKIMWI. Kufuatia mabadiliko hayo, Serikali inachukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uwekezaji kwenye eneo la utaoji huduma kwa WAVIU.
“Hatua hizo zenye lengo la kuwezesha Taifa letu kujitegemea zitaendelea kuchukuliwa pia katika maeneo mengine. Niwahakikishie Watanzania wote, kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma zinazohusiana na masuala ya UKIMWI zinaendelea kupatikana na hakuna Mtanzania atakayekosa huduma hizo”- amesema Waziri Majaliwa