Asilimia 63 ya madaktari hawafati miongozo iliyowekwa.

Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na Wizara ya Afya nchini Tanzania imebaini kuwa asilimia 63 ya madaktari katika hospitali za rufaa za mikoa nchini humo hawafuati miongozo iliyowekwa ikiwamo kuchukua historia ya mgonjwa.

Mfumo wa Tehama ‘IT’ umeonyesha ni asilimia 37 pekee ya madaktari ambao wamekuwa wakiuliza wagonjwa wanaowatibu na kujaza historia zao huku wakiwapa maelezo mbalimbali muhimu ikiwamo kwanini wanawapima na umuhimu wa kutumia dawa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi wakati akifungua mkutano wa viongozi wa vyama vya kitaaluma nchini uliozungumzia uboreshaji wa huduma za afya nchini, uwajibikaji na maadili ya watumishi wa afya.

“Katika utoaji huduma kuna utaratibu na vyuoni inafundishwa daktari, mgonjwa akishapita kwako unampima na kuchukua historia yake takwimu zinaonyesha ni asilimia 27 pekee ya madaktari wetu hospitali za rufaa za mikoa wanachukua historia ya mgonjwa mfumo wa IT umeonyesha,” amesema.

Pia amesema asilimia kubwa wamekuwa hawawaelezi wagonjwa kuhusu tiba wanazotoa na kwanini ni muhimu mgonjwa kupima kipimo anachomwandikia na sababu iliyopelekea kuandika hicho kipimo.

“Wengi anaandika tu diagnosis ‘alichokibaini’ anaingiza na vipimo kwa kuwa ni lazima ziingizwe maabara mgonjwa apate dawa. Wanataaluma tukakumbushane na hili huenda hospitali binafsi lipo zaidi hali inaweza kuwa hivyohivyo.

“Unampa dawa za presha miezi 6 humfuatilii inaweza kuleta tatizo kwenye ini, figo dawa za muda mrefu bila kumwangalia vizuri inabidi uwe na majibu anavyoendelea umwangalie kwa macho, vipimo na kubaini hali yake inavyoendelea,” amesema Profesa Makubi.

Amesema katika ukaguzi ambao unatarajiwa kufanywa wataangalia suala hilo na litakuwa zoezi shirikishi.

“Tuliangalia pia kwenye famasi, mawasiliano ya wagonjwa na daktari imekua changamoto hasa katika kutoa mrejesho. Watumishi wa sekta ya afya ni wagumu kumwelezea mgonjwa kwanini unampima na itasaidia nini na kwanini unampa dawa fulani mrejesho ni changamoto kubwa,” amesema.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe ametoa wito kwa wasimamiaji wa huduma kuhakikisha wanafuata ubora wa huduma kwa wananchi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuzuilika ikiwemo vifo.

Kwa upande mwingine, Dk Sichalwe ametoa wito kwa wanataaluma kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa (surveillance) ili kutambua mapema magonjwa, ikiwamo magonjwa ya mlipuko na kuweka mikakati mizuri ya namna bora ya kupambana dhidi ya magonjwa hayo kwa kushirikiana na Serikali.

Msajili wa Baraza la famasia, Elizabeth Shekalaghe ametoa wito kwa wanataaluma wa afya nchini kuhakikisha wanazingatia sharia, kanuni na miongozo katika utendaji kazi wao.