Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela askari polisi namba 4987, Sajenti Rogers Mmaly, aliyekuwa akihudumu katika Kituo cha Polisi Ipogolo, Manispaa ya Iringa, baada ya kupatikana na hatia ya kusababisha kifo cha Nashon Kiyeyeu.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Angaza Mwipopo baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri. Akisoma hukumu, Jaji Mwipopo amesema kuwa ushahidi uliotolewa ulithibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 14, 2024 katika eneo la Ipogolo.
Kwa mujibu wa mahakama, marehemu alipatikana na majeraha mbalimbali mwilini yaliyosababishwa na kipigo cha kitu chenye ncha kali, pamoja na kupasuka kichwa hali iliyosababisha kuganda kwa damu kwenye ubongo upande wa juu wa kulia.
Aidha, mahakama ilieleza kuwa baada ya tukio hilo, mshtakiwa alikimbilia Moshi kwa lengo la kupoteza ushahidi, kabla ya kukamatwa na kurejeshwa Iringa kwa ajili ya kuendelea na mwenendo wa kesi hiyo.
Ushahidi wa mazingira uliwasilishwa mahakamani ulionyesha kuwa marehemu alionekana kwa mara ya mwisho akiwa na mshtakiwa ndani ya gari lake aina ya Noah. Pia ilibainika kuwa mshtakiwa alishindwa kufungua jalada la kesi kuhusiana na tuhuma za wizi wa simu ya mkononi iliyodaiwa kuibwa kwa Beatrice Kimata.
Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa kwa mujibu wa vifungu namba 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kwa kosa la kuua bila kukusudia. Ilielezwa kuwa mshtakiwa alikiri kumpiga marehemu akidai alimjibu vibaya wakati wa mahojiano, kitendo kilichosababisha kifo hicho.
Jumla ya mashahidi sita kutoka upande wa Jamhuri waliwasilisha ushahidi uliosaidia mahakama kufikia uamuzi huo.
Katika hatua nyingine, wakili wa utetezi, Cleofas Mheluka, aliiomba mahakama kupunguza adhabu akieleza kuwa mshtakiwa ana familia yenye watoto watano na anakabiliwa na matatizo ya kiafya, huku akisisitiza kuwa tukio hilo halikuwa la kukusudia.
Hata hivyo, baba wa marehemu, Nashon Kiyeyeu, amesema hajaridhishwa na hukumu hiyo, akidai kuwa kitendo hicho kilifanywa kwa makusudi na kuiomba serikali kuingilia kati ili haki itendeke kikamilifu.