Askofu Gwajima ajiripua..aibua orodha ya Waliotekwa, ataka mabadiliko ya mfumo wa Usalama

Mbunge wa Jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima, ameibua hoja nzito kuhusu mustakabali wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini, akisisitiza haja ya kuwepo kwa mfumo huru na wa kitaasisi wa uteuzi wa wakuu wa vyombo hivyo, ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa ufanisi bila kuingiliwa na wanasiasa.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi Mei 24, 2025, Gwajima alitumia majukwaa hayo kulaani vikali vitendo vya utekaji vinavyoripotiwa nchini, akisema vinaathiri taswira ya Tanzania kitaifa na kimataifa, na kuvichafua vyombo vya dola visivyo na hatia katika baadhi ya matukio.

Katika kauli yake yenye msisitizo, Gwajima alisema Ushauri wangu, wakuu wa vyombo vya usalama ili wafanye kazi zao kwa umahiri, wasiondolewe kwenye kazi zao kwa mapenzi ya mwanasiasa aliyewaweka. Hii itawapa uwezo wa kukataa baadhi ya maagizo yasiyo na maslahi kwa nchi.”

Ameonya kuwa mfumo wa sasa wa uteuzi na uondoshaji wa viongozi wa vyombo vya ulinzi kwa misingi ya kisiasa unavifanya vyombo hivyo kupoteza uhuru na weledi, hali inayofifisha uwezo wake wa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya matendo yanayohatarisha usalama wa taifa.

Kuhusu Vitendo vya Utekaji nchini

Mbunge huyo ambaye pia ni kiongozi wa dini, ameibua msururu wa matukio ya utekaji wa raia, akisisitiza kuwa vitendo hivyo haviendani na utamaduni wa Tanzania. Ameeleza kuwa amekuwa akipokea taarifa za matukio ya utekaji, ambapo amesema kuna orodha ya takribani watu 83 waliowahi kutekwa katika miaka ya hivi karibuni.

“Utekaji si utamaduni wa Tanzania. Tumeona watu wanachukuliwa mbele ya familia zao, wengine wanapotea, wengine wanarudishwa wakiwa wamejeruhiwa au wamepoteza maisha. Hili si jambo dogo na linaumiza taifa,” alisema Gwajima kwa masikitiko.

Akitolea mfano kifo cha mwanachama wa Chadema Ally Kibao ambaye aliuawa muda mfupi baada ya kushuhswa kwenye basi lililokuwa likielekea Tanga Gwajima alisema “Alishushwa kwenye gari mchana kweupe mbele ya watu, kesho yake akapatikana amekufa. Haya matukio ni ya kushtua na kutisha. Kama ingekuwa baba yako amepatwa na hayo ungesemaje?”

Kadhalika Gwajima amekemea tukio la kukamatwa kwa mwanaharakati na mwanachama wa CHADEMA Mdude Nyagali, ambaye alichukuliwa nyumbani kwake mbele ya mke wake na watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi 

“Tumeona juzi kule Mtu anaitwa Mdude ambaye na yeye Watu wamekuja nyumbani kwake wamevunja mlango wamemchukua akiwa hai mbele ya Familia yake wameondoka nae mpaka leo hatujui yuko wapi na hatujui nani anafuata unaweza kunyamaza kumbe unafuata wewe, kwahiyo haya mambo yamezidi kipimo na lengo langu leo kusema haya mambo na kutoa ushauri”

Vitendo vya udhalilishaji kwa Wanaharakati wa ndani na nje

Gwajima pia alieleza wasiwasi wake juu ya matukio ya udhalilishaji yanayowakumba wanaharakati kutoka nje ya nchi wanapokuwa Tanzania, akimtolea mfano mwanaharakati wa Uganda, Agather, aliyedaiwa kudhalilishwa na watu waliodai kuwa ni wa vyombo vya usalama kabla ya kutupwa mpakani.

Aidha, aliukumbusha umma kuhusu tukio la mwanaharakati wa Kenya, Boniface Mwangi, ambaye alidai kuchukuliwa katika Hoteli ya Serena na baadaye kuokotwa mpakani, akisema:
“Juzijuzi hapa Mwanaharakati wa Uganda Msichana anaitwa Agather wamekuja kwenye shughuli zao kuhudhuria Mahakamani amechukuliwa na Watu waliojitambulisha ni Watu wa Vyombo Mimi sina uhakika kama ni Watu wa Vyombo nimeona anaongea Youtube kwa uchungu kwamba kaenda mahali akavuliwa nguo kafanyiwa udhalilishaji akaenda kutupwa mpakani, sasa tujaribu kuwaza kama angekuwa ni Mama yako mzazi amechukuliwa anavuliwa nguo anadhalilishwa anatupwa mahali ungejisikiaje au angekuwa Dada yako?, ni akina nani hawa wenye ujasiri”

“Boniface Mwangi Mwanaharakati wa Kenya tumemuona Serena Hotel Watu waliojitambulisha ni Watu wa Vyombo wameenda nae baadaye Mtu anaokotwa mpakani, sasa kunakuwa na picha gani?, Mimi siamini kabisa kama kuna Vyombo Tanzania kwa maana ya Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa au Chombo chochote Dola kinaweza kufanya kazi ya namna hii, Chombo cha Dola mnaenda kujitambulisha ni Watu wa chombo mkamchukua Mtu kwenda kumtupa si watasema ni nyinyi”

“Matukio haya yanapohusishwa na vyombo vya usalama, hata kama si kweli, yanaathiri taswira ya vyombo vyetu. Tunaharibu heshima yetu mbele ya macho ya dunia.”

Wito kwa Wananchi na Wanachama wa CCM

Gwajima alisisitiza kuwa yeye ni mwanachama wa CCM lakini hatakubali kunyamaza mbele ya matendo yanayokiuka misingi ya haki na utu.
“Anayesema mimi napinga CCM nimwulize, je, CCM tunakubali utekaji? MwanaCCM wa kweli lazima apinge jambo hili.”

Gwajima alieleza kuwa vitendo vya utekaji vinapoendelea huku baadhi ya wahusika wakihusishwa na kauli kama “sema asante Samia” vinaathiri heshima ya Rais na mahusiano ya kidiplomasia.

“Mahusiano ya nchi na nchi yakivurugika, biashara itakwendaje? Wenye makampuni wataogopa kuja, utalii utayumba. Sasa tupo kimya kwa sababu gani?” alihoji kwa sauti ya majonzi.