Askofu Shoo aweka imani yake kwa Dk Tulia

Askofu Fredrick Shoo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini Tanzania (KKKT)

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amesema Bunge la Tanzania lilifika mahali lilionekana kuwa dhaifu na kwamba kwa sasa ana imani kuwa  Dk Tulia Akson akiwa spika atarudisha heshima ya Bunge.

Amesema ilifika mahali Bunge limeonekana kuwa dhaifu na kupoteza heshima yake na kwamba kwa sasa matarajio makubwa ni kwamba Bunge linakwenda kusimama katika nafasi yake ya kuisimamia serikali, kuishauri na mijadala itakayotolewa kuwa yenye staha na si mahali pa kebehi wala ubabe.

Askofu Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, ameyasema hayo leo Ijumaa wakati akizungumza na wanahabari mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kuhusiana na maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitisha jina moja la mgombea wa nafasi ya uspika.

“Nina imani kubwa na mgombea wa nafasi ya spika ambaye Chama cha Mapinduzi kimependekeza jina lake. Kikubwa, Spika ajae tunamtarajia atunze heshima ya Bunge, kwani ilifika mahali Bunge kweli lilionekana kuwa dhaifu na pia pakawa mahali ambapo wabunge wenyewe hawajaweza kutunza heshima ya kile chombo jinsi ambavyo inavyotarajiwa,” alisema Askofu Shoo.

Askofu Shoo amesema Bunge ni chombo kitukufu na ni mahali ambapo panahitajika heshima ikiwa pamoja na wabunge wenyewe kupaheshimu na mijadala iwe yenye staha badala ya kebehi na kuonyeshana ubabe.

“Kutunza heshima ya Bunge na uhuru wa Bunge, kwa mujibu wa katiba yetu, kwamba kiwe chombo cha kuisimamia serikali lakini pia kuishauri serikali na natarajia na namwombea spika ajaye asimamie mambo hayo,” amesema.

Akizungumzia CCM kuja na jina moja la mgombea uspika miongozi mwa wale 70 waliorejesha fomu, Dk Shoo amesema ni hekima na busara na inaonyesha dhahiri kuwa wamekubaliana mgombea huyo mmpoja apitishwe ili aweze kugombea na wagombea wengine watakaosimama kugombea nafasi hiyo Bungeni.

“CCM kuteua jina moja la Tulia Akson, wametumia hekima na busara kubwa, kwa sababu bila shaka wameangalia katika wale wote 71 waliochukua fomu za kutaka kugombea kiti hicho ni nani mwenye uwezo, uzoefu na ni nani anayekubalika,” amesema.

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM jana ilipitisha jina pekee la Dk Tulia Ackson kuwa mgombea wa kiti cha Spika kilichoachwa wazi na Job Ndugai, aliyejiuluzu nafasi hiyo Januari 6, 2022.

Uratibu wa CCM ni kupeleka majina yasiyozidi matatu kwenye kamati ya wabunge. Wanaweza kupeleka moja au mawili au matatu.