Katika ripoti yake ya awali, Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa AU ulisema kuwa baadhi ya wapiga kura walipatiwa karatasi nyingi za kupigia kura, na wengine waliruhusiwa kupiga kura bila majina yao kuthibitishwa kwenye daftari la wapiga kura.

Ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU) umeeleza kuwa uadilifu wa uchaguzi mkuu wa Tanzania uliomalizika hivi karibuni “ulivurugwa”, baada ya kuripotiwa visa vya “kujaza kura kwa wingi katika vituo kadhaa vya kupigia kura.”
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rais Samia Suluhu Hassan alishinda uchaguzi wa Oktoba 29 kwa asilimia 98 ya kura, lakini upinzani ambao ulizuiwa kushiriki umeutaja uchaguzi huo kuwa “batili.”
Siku ya uchaguzi zilisheheni machafuko katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali ilijibu kwa kuzima intaneti kwa muda wote na kusimamisha usafiri, huku vyama vya upinzani vikidai kuwa mamia ya watu waliuawa na vikosi vya usalama. Hata hivyo, ni vigumu kuthibitisha idadi kamili kutokana na vizuizi vya taarifa, licha ya kupungua kwa baadhi ya vikwazo.
Katika ripoti yake ya awali, Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa AU ulisema kuwa baadhi ya wapiga kura walipatiwa karatasi nyingi za kupigia kura, na wengine waliruhusiwa kupiga kura bila majina yao kuthibitishwa kwenye daftari la wapiga kura.
“Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025 haukukidhi kanuni, mifumo ya kimaadili ya AU, wala wajibu wa kimataifa na viwango vya uchaguzi wa kidemokrasia,” ilisema ripoti hiyo ya awali ya AU.
Waangalizi walisema walizuiwa kushuhudia zoezi la kuhesabu kura, jambo lililopunguza uwazi wa mchakato huo. Baadhi yao walisema waliagizwa “kuangalia tu upigaji kura kwa dakika tano” katika vituo fulani.

Ripoti hiyo pia iliorodhesha matukio ya maandamano ya vurugu, milio ya risasi, kufungwa kwa barabara, na kuchomwa kwa matairi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kagera, Dodoma, Kigoma, Tabora, Buhungwa, na Singida.
AU imetoa wito kwa Tanzania “kuzipa kipaumbele mageuzi ya kisiasa na ya uchaguzi ili kushughulikia mizizi ya changamoto zake za kidemokrasia na kiuchaguzi.”
Novemba 3, 2025 siku ya Jumatatu, waangalizi wengine wa uchaguzi wa bara hilo walitoa ripoti ya awali wakisema kuwa Watanzania hawakuweza “kuonesha matakwa yao ya kidemokrasia” kutokana na kuwekewa vikwazo vya ushiriki wa wagombea wa upinzani, udhibiti wa habari, vitisho, na dalili za wizi wa kura siku ya uchaguzi.