Kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 18 hadi 22 ameuawa na mwili wake kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali waliodai kuwa kuwa alijaribu kutaka kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari iliyopo Kata ya Bombambili mjini Geita.
Tukio hilo limetokea Februari 24, 2022, majira ya asubuhi wakati mwanafunzi huyo akiwa njiani kwenda shule.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa mwanafunzi huyo alitoka nyumbani alfajiri kuwahi shuleni, lakini akiwa njiani ndipo alipokamatwa na kijana huyo akimvutia kichakani kwa lengo la kumbaka.
Amesema kijana huyo alipomkamata mwanafunzi huyo alipiga kelele na wananchi walikusanyika na kumzingira ndipo walianza kumuokoa mwanafunzi na kumpeleka shule kisha kumshambulia kijana huyo hadi kumuua na mwili wake kuchomwa moto.
Kufuatia tukio hilo Kamanda Mwaibambe amesema jeshi la Polisi linamshikilia Mwenyekiti wa mtaa huo Salum Maige ili kusaidia kufahamika kwa wote waliohusika kwenye mauji hayo.
“Marehemu alishazingirwa hatuoni sababu za kumuua zaidi ya kumfikisha kwenye vyombo vya sheria. Kwa kuwa mauaji yamefanywa na wananchi wa eneo hilo tunamshikilia mwenyekiti ili asaidie polisi kuwapata wahusika,” amesema Kamanda Mwaibambe.