Mkulima mkazi wa kijiji cha Basanza wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma amefariki dunia baada ya kulipuliwa na bomu la kurusha kwa mkono lililorushwa ndani ya kilabu cha pombe wakati akinywa na wenzake.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu alisema kuwa aliyeuawa kwenye tukio hilo ni Amos Petro (45) na watu wengine wawili walijeruhiwa.
Kamanda Makungu alisema Petro alifariki dunia kwenye Hospitali ya Wilaya Uvinza wakati akipata matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya mguu wa kushoto na kuvuja damu nyingi.
Aidha kamanda Makungu aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Juma Omari (51) na Sara Misigaro wakazi wa kijiji cha Basanza ambao wako hospitali ya wilaya Kasulu wakipatiwa matibabu.
Kamanda Makungu alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo mtu mmoja alirusha bomu hilo kwenye kilabu cha pombe za kienyeji wakati Petro na wenzake wakinywa pombe.
Alisema uchunguzi wa awali umeonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia na hivyo upelelezi unaendelea ili kuwakamata na kuwachukulia hatua wanaohusika.