FIFA imeendeleza msukumo wake wa kutaka kuandaa Kombe la Dunia la wanaume kila baada ya miaka miwili kwa kupata uungwaji mkono na mashabiki wa kandanda kote duniani. Mashabiki hao wakiwa wamepigia debe kufanyika kwa shindano la Kombe la Dunia kwa kupiga kura kupitia mtandao.
Shirika la kandanda kutoka Uropa, UEFA na lile la kutoka Amerika Kusini CONMEBOL, yanapinga mpango huo wa FIFA na wametishia kususia kushiriki katika mashindano yajayo ya Kombe la Dunia.
Mabara ya Ulaya na Amerika Kusini yanajumla ya wanachama 65 kati ya 211 wanachama wa FIFA kutoka mabara mengine, ikiwa ni chini ya thuluthi moja ya kura zinazohitajika kuzuia azimio la FIFA.
Kila bodi katika mabara 6 duniani husimamia maandalizi ya mashindano ya kandanda katika mabara yao. Bodi ya kandanda Ulaya ikiandaa mashindano yake kila baada ya miaka minne katikati ya maandalizi ya Kombe la Dunia. Kuandaliwa kwa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili huenda kukapunguza mapato ya ligi ya Uropa.
Rais wa FIFA Gianni Infantino anaamini kuandaa mashindano zaidi ya Kombe la Dunia kutayapa fursa mataifa 211 wanachama wa FIFA nafasi zaidi za kushiriki katika mashindano ya Kombe la Dunia hususan mataifa mengi ambayo hayajawahi kufuzu kushiriki mashindano hayo.
Kuongeza idadi ya mataifa yanayoshiriki katika Kombe la Dunia kutoka mataifa 32 hadi 48 kuanzia mashindano ya 2026 ulikuwa uamuzi wa kwanza wake Gianni Infantino kama rais wa FIFA, uamuzi huo aliufanya 2016. FIFA pia inapanga kusambaza fedha zinazotokana na kuandaliwa kwa mashindano ya Kombe la Dunia kukuza talanta na kusaidia timu za kitaifa duniani kutoka mabara mengine kufikia viwango vya talanta kama vile vya Ulaya.
Timu za Ulaya zimeshinda mashindano 4 ya mwisho ya Kombe la Dunia na kuchukua nafasi 13 kati ya 16 za semifainali, nafasi 3 kati ya hizo zikichukuliwa na mataifa ya Amerika Kusini.