Baba wa kijana aliyechoma picha ya Rais aomba kupatikana kwa mwanawe akiwa hai au mfu

Yusuph Chaula ambaye ni baba mzazi wa Shadrack Chaula amemuomba Rais Samia kuingilia kati suala la mwanawe Shedrack Chaula anaedaiwa kutekwa na watu wasoijulikana.

Shadrack Chaula anadaiwa kutekwa Agosti 2, 2024 ikiwa ni takribani siku 20 kupita tangu alipotoka Gereza la Ruanda lililoko mkoani Mbeya.

Shedrack mwenye umri wa miaka 24 mnamo Julai 4,2024 alitiwa hatiani na Mahakama ya wilaya ya Rungwe mkoani Rungwe kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa TikTok, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya makaosa ya mtandao kifungu cha 16.

Baba mzazi wa Shedrack, ameeleza kuwa Shedrack alibebwa kwa nguvu na watu wasiojulikana na kuingizwa kwenye gari nyeusi kisha gari hiyo ikaelekea jijini Mbeya.

Hadi sasa hajui mtoto wake yupo wapi licha ya jitihada mbalimbali za kumtafuta kwa ndugu, jamaa na marafiki hadi hospitalini lakini jitihada zake hazikuzaa matunda hivyo ameliomba jeshi la polisi kufanya jitihada za kumtafuta mtoto wake apelekewe akiwa hai au amekufa.

“Awali mwanangu nikiri kwamba alifanya ukorofi, baada ya kufanya kosa la kuchoma picha ya kiongozi Mkuu wa nchi, sheria zilitenda haki alihukumiwa miaka miwili katika Mahakama ya Rungwe”- Baba mzazi wa Shedrack

 Katika hukumu hiyo mahakama ilimtaka kulipa faini ya shilingi milioni 5 ambayo ilitolewa kupitia michango iliyotolewa na Watanzania na alifanikiwa kutoka gerezani baada ya kukaa siku kadhaa.

Shedrack anajishughulisha na shughuli za uchoraji lakini mbali na hilo pia ni mfanyabiashara wa duka.