Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe amesema Serikali haijazuia watu kufanya biashara ya kuuza mazao nje ya nchi, badala yake kilichozuiwa ni watu kufanya biashara bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Bashe amesimama bungeni kutoa msimamo huo wa Serikali kufuatia uwepo wa hoja za wabunge mbalimbali wakieleza kuwa Serikali imeweka zuio hilo.
“Haiwezekani mtu unanunua mahindi Songea, unayapakia kwenye lori huna business license [leseni ya biashara] ya aina yoyote, hata business name [jina la kibiashara], huna TIN [Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi], huna tax clearance [kibali cha kodi] huna export permit [kibali cha kusafirisha bidhaa nje] halafu unataka nchi ikuruhusu kwenda kuuza nje mazao hayo,” amehoji Waziri Bashe.
Amesema usafirishaji bubu wa mazao nje unasababisha matatizo mbalimbali ikiwemo malipo kutoonekana kwenye mfumo rasmi wa fedha na nchi kukosa takwimu za usafirishaji wa mazao nje.
“Nia ya Serikali ni kurasimisha shughuli za kilimo na shughuli za kibiashara za mazao,” ameeleza Bashe huku akiwataka wale wote wanaotaka kufanya biashara hiyo kwenda kujirasimisha kwenye halmashauri na mamlaka husika.
Akitoa taarifa kuhusu hoja ya Mbunge wa Lupembe, Edwin Swalle kuhusu urasimu kwenye upatikanaji wa vibali na leseni hizo, Waziri Bashe amesema kuanzia Julai Mosi mwaka huu wale wote watakaokuwa na leseni za biashara wataanza kupata vibali/leseni za kusafirisha mazao nje kwa njia ya mtandao hivyo kuondoa adha inayowakabili wafanyabiashara.