Bashe:Tanzania haina njaa

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe, amekanusha uwepo wa baa la njaa nchini humo lakini amekiri kupanda kwa bei za mazao.

Bashe amesema bei ya mazao imepanda kwasababu ya maamuzi ya Rais wa nchi hiyo kuifanya sekta ya kilimo kuwa sekta ya kibiashara.

Waziri huyo ametoa kauli hiyo leo 23 Novemba, 2022, katika ziara ya Rais Samia Suluhu mkoani Manyara.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kujiwekea akiba ya chakula ambapo amesema Serikali imeendelea na jitihada za kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kutoka tani 200,000 kufika tani laki 500,000.

Jana Rais Samia alishuhudiwa akizindua vihenge vikubwa vya kuhifadhia nafaka ambavyo vitasaidia kuongeza uwezo wa hifadhi ya Taifa ya chakula.

Bashe amesema bei ya chakula inapopanda Serikali hutumia hifadhi iliyopo kuongeza upatikanaji ili kupunguza ushindani kwenye soko na hivyo bei kupungua.

“Leo nimezunguka hapa babati b=debe la mahindi limefika Sh 20,000, Serikali inachofanya ni kuchukua mazao na kupeleka sokoni na kuuza kwa bei ya chini. Tutafanya hivyo, tutakifungulia,” amesema.

Amefafanua kuwa wataalamu wa kilimo wanafanya tathimini na kwamba watauza mahindi katika maeneo maalumu kwa bei ya rejareja na si kwa wafanyabiashara wakubwa.

Amesema mahindi hayo yatauzwa kwa bei ya Sh 700-800 kwa kilo sawa na Sh 14,000-15000 kwa debe moja la mahindi.

“Serikali kazi yake sio kuua soko bali kufanya hatua ambazo zitafanya wananchi wapate unafuu bila kumtia umasikini mkulima,” amesema.