BAWACHA wampokea kwa shangwe Rais Samia kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani

Rais Samia Suluhu Hassan amehudhuria maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, yalioandaliwa na Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA).

Maadhimisho hayo ambayo Bawacha wanafanya Kitaifa mjini Moshi katika Ukumbi wa Kuringe pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama vya siasa.

Wakati Rais Samia akiingia ukumbini hapo amepolewa na mabango yenye jumbe mabalimbali ikiwemo ‘Katiba Mpya ni Sasa, Wanawake tunataka katiba mpya kabla ya 2025,  miaka 7 ya kufungwa mdomo imeisha, maridhiano yaendelee, tunapinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, na lile lililoandikwa Wahanga wa zao la korosho bei hafifu na pembejeo hafifu.

Wanawake hao pia wanatarajia kumueleza Rais changamoto mbalimbali zinazowakabili hapa nchini, ambapo wanaamini zitapata utatuzi

Viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu pamoja na viongozi wengine wa dini akiwemo Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo.

Mbali na viongozi hao wa serikali na dini, pia wapo viongozi wakuu wa Kitaifa wa Chadema akiwemo, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa,  Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Katibu Mkuu Bawacha, Catherine Ruge, Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Sharifa Suleiman pamoja na viongozi wengine wa siasa wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro.