Bei ya Mafuta ya Petroli na Dizeli yapanda nchini Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za rejareja za nishati hiyo ambazo mwezi huu zimepanda ikilinganishwa na Februari 2022.

Ewura imetangaza bei hizo leo kuhusu bei za mafuta zitakazoanza kutumika kesho, imeainisha kuwa huenda gharama za mafuta zingekuwa juu zaidi kama Serikali isingeahirisha kodi ya shilingi 100 kwa kila lita moja ya mafuta.

Hivyo mafuta yatakayopitia bandari ya Dar es Salaam, yatauzwa kwa bei pungufu ya shilingi 100 kwa miezi mitatu mfululizo.

Kuanzia kesho Petroli itauzwa kwa shilingi 2,540 ikiwa imepanda kwa shilingi 60 kutoka shilingi 2,480 ya mwezi Februari, huku  dizeli ikiuzwa shilingi 2403 ikipanda kutoka shilingi  2,338.

Hata hivyo, mafuta ya taa yameshuka hadi kufikia shilingi 2,208 kutoka shilingi 2,291. 

Maumivu hayo pia yatawagusa watumiaji wa nishati hiyo wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, inayopokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda. 

Kwa Machi 2022, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa tarehe 2 Februari 2022.

Kwa Machi 2022, bei za rejareja za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa shilingi 165/lita (sawa na asilimia 6.88) na shilingi 207/lita (sawa na asilimia 9.09), mtawalia. Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa shilingi 164.76/Lita (sawa na asilimia 7.26) na shilingi 206.62/lita (sawa na asilimia 9.62), mtawalia.

Kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye matanki ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya Taa Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za Mafuta ya Taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea Mafuta ya Taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika

Pia bei za rejareja za mafuta ya petroli katika mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zimeongezeka ambapo petroli itauzwa kwa Sh2,577, dizeli Sh2,530 na mafuta ya taa kwa Sh2,280.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba jana alitangaza kuahirisha ukusanyaji wa tozo ya shilingi 100 kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa kipindi cha miezi mitatu tangu jana alipotoa tangazo hilo.

Tozo hiyo ilipaswa kulipwa na watumiaji wa mafuta nchini humo kuanzia mwezi Machi mpaka Mei, mwaka huu huku taifa likiendelea kutathmini mwenendo wa soko la dunia katika mafuta.

Hatua hiyo, itaifanya Serikali kukosa shilingi bilioni 30 kila mwezi.  Uamuzi huo umekuja kutokana na kupanda bei za mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na vita kati ya Urusi na Ukraine.