Bei ya Petroli yashuka kiduchu

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za mafuta ya petroli na dizeli ambazo zimeanza kutumika leo Juni 05,2024.

Kwa mwezi huu wa Juni bei ya rejareja ya mafuta ya petroli kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa shilingi 53 na kufikia shilingi 3,261 kwa lita moja, ikilinganishwa na bei ya mwezi Mei iliyokuwa shilingi 3,314.

Dizeli inauzwa shilingi 3,112 tofauti ya shilingi 84 ambapo mwezi Mei iliuzwa shilingi 3,196.

Mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Juni 2024 kulinganisha na mwezi Mei, 2024 yamechangiwa na kupungua kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 11.82 kwa mafuta ya petroli, asilimia 7.77 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 7.94 kwa mafuta ya taa.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa asilimia 1.4, kupungua kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 2.06 kwa petroli na asilimia 8.51 kwa dizeli katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 7.07 kwa petroli na asilimia 25.24 kwa dizeli katika Bandari ya Tanga.