Benki Kuu ya Tanzania yaiweka chini ya uangalizi benki ya Yetu Microfinance 

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeiweka Benki ya Yetu Microfinance chini ya uangalizi wake ili kulinda haki za wateja na wadau wengine, kutokana na benki hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji wa ukwasi.

Taarifa iliyotolewa Desemba 12, 2022 na Gavana wa BoT, Profesa Florens imesema usimamizi huo umeanza mara moja na utadumu kwa siku zisizozidi 90 kabla ya kutoa majumuisho.

“Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na Benki ya Yetu Microfinance kuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji kinyume na matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake unaohatarisha usalama wa sekta ya fedha,” amesema Gavana Luoga.

BoT imefanya uamuzi huo kwa mamlaka iliyonayo chini ya Kifungu cha 56 (1)(g)(i) na (iii) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Sambamba na usimamizi wa shughuli za benki hiyo ambayo imesitishiwa kutoa huduma, BoT imeisimamisha bodi ya wakurugenzi na menejimenti na kumteua meneja wa muda atakayeratibu shughuli zake kwa kipindi chote cha usimamizi.

“Benki ya Yetu Microfinance kuendelea kutoa huduma za kibenki, kutahatarisha usalama wa amana za wateja wake. Hivyo basi, Benki Kuu ya Tanzania imemteua meneja msimamizi. Umma unaarifiwa kuwa katika kipindi kisichozidi siku 90 kuanzia siku ya taarifa hii, utoaji wa huduma za kibenki za Benki ya Yetu Microfinance utasimama ili kuipa nafasi Benki Kuu kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili,” amesema Profesa Luoga

Licha ya kuisimamisha bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya Benki ya yetu Microfinance kuanzia leo, BoT imewahakikishia wateja, wanahisa na umma wa Watanzania kwa ujumla kwamba itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika benki na taasisi za fedha kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

Hivi karibuni Serikali imekuwa ikisisitiza benki kuungana ili zibaki chache zitakazotoa huduma za uhakika kwa wananchi wengi zaidi. 

Katika kuhakikisha hilo, imekuwa ikiziwezesha benki zenye changamoto za ukwasi au mtaji kuungana na zilizo imara.

Mwaka 2017, BoT iliifunga Mbinga Community Bank kutokana na sababu hizo na mwaka uliofuatia, yaani 2018 ikazifunga nyingine tano ambazo ni Efatha, Covenant Bank for Women (Tanzania), Njombe Community Bank, Kagera Farmers’ Cooperative Bank na Meru Community Bank.

Huo haukuwa mwisho, mapema mwaka 2020, BoT iliziunganisha Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na Benki ya Posta (TPB) muungan uliozalisha Benki ya Biashara Tanzania (TCB).