Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amesusia kuanza kwa kesi yake ya muda mrefu ya uhaini siku ya Jumatatu, akimtuhumu jaji anayesikiliza kesi hiyo kuwa na upendeleo na upande mmoja wa mashtaka.
Besigye, mwenye umri wa miaka 69, ni mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miaka 40 na amewahi kushindana naye bila mafanikio katika chaguzi nne.
Alitekwa nyara nchini Kenya mnamo Novemba na kurejeshwa Uganda ambako anakabiliwa na adhabu ya kifo kwa mashtaka ya uhaini, mashtaka ambayo yamekosolewa vikali na makundi ya kimataifa ya haki za binadamu.
Kesi yake ilipaswa kuanza Jumatatu, lakini yeye na mwenzake Obeid Lutale “walikataa kufika mahakamani… kwa sababu wanaamini hawatapata usikilizwaji wa haki,” mmoja wa mawakili wao, Erias Lukwago alisema.
“Wameomba mahakama Jaji Emmanuel Baguma ajiondoe katika kesi hiyo lakini amekataa, hivyo wameamua kutofika mbele yake hadi jaji mwingine atakapoteuliwa,” aliongeza wakili huyo
Watuhumiwa wanasema jaji huyo ana upendeleo kwa sababu alikataa kuwapa dhamana.
Kwa mujibu wa sheria za Uganda, mtuhumiwa hawezi kuzuiliwa bila kushtakiwa kwa zaidi ya miezi sita, lakini mwezi uliopita jaji aliamua kuwa muda huo ulianza kuhesabiwa Februari wakati mashtaka yaliposomwa rasmi, badala ya wakati
-Besigye alipotekwa na kupelekwa gerezani kijeshi-
Mawakili wake waliita uamuzi huo “wa ajabu”.Makundi ya haki za binadamu yamehusisha utekaji na kesi ya Besigye na uchaguzi wa Januari ujao ambapo Museveni, mwenye umri wa miaka 80, atagombea muhula mwingine madarakani.
Mwezi Juni, mke wa Besigye, Winnie Byanyima ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS alisema mumewe anazuiliwa “kwa sababu za kisiasa” na katika mazingira “yasiyo ya kibinadamu”.
Kesi ya Besigye hapo awali ilisikilizwa na mahakama ya kijeshi, lakini baadaye ikahamishwa hadi mahakama ya kiraia baada ya Mahakama ya Juu kuamua kuwa ni kinyume cha katiba kuwahukumu raia katika mahakama za kijeshi.
Hata hivyo, baadaye Museveni alisaini sheria mpya inayorejesha mashitaka ya kiraia katika mahakama za kijeshi chini ya kile kilichoelezwa kama “mazingira maalum”.