Biashara ya ngono yaongezeka kwa wakimbizi wa ndani DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi UNHCR limetoa wito wa kuwasaidia wakimbizi walioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC ambao wapo katika hali mbaya kutokana na kuendelea kwa machafuko yanayofanywa na makundi yenye silaha hali inayofanya watu kuyakimbia makazi yao.

Taarifa iliyotolewa jana na shirika hilo kutoka Geneva Uswisi imesema ukosefu wa amani huko mashariki mwa DRC umesababisha watu kuwa na hali mbaya ya kimaisha na ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, unaowakabiliwa zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 6.2.

Ili kufahamu ukubwa wa mgogoro na kutafuta fursa za kuboresha usaidizi wa kuokoa maisha kwa watu waliokimbia makazi yao huko mashariki mwa DRC, wiki hii Kamishna Mkuu Msaidizi wa Ulinzi wa UNHCR Gillian Triggs na Kamishna Mkuu Msaidizi wa Operesheni Raouf Mazou walitembelea nchi hiyo na kujionea changamoto zinazowakabiliwa wakimbizi.

Beni

Wakiwa mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini viongozi hao wa UNHCR walikutana na kuzungumza na wakimbizi wa ndani waliorejea na kupatiwa usaidizi na shirika hilo pamoja na washirika wengine wa masuala ya kibinadamu.

Pamoja na usaidizi waliopatikwa bado wanakabiliwa na changamoto lukuki. Wanawake walieleza changamoto kubwa ni kupata chakula cha kulisha familia zao kwani machafuko yanakatisha uwezo wao wa kulima na hivyo kushindwa kupata mlo wala kujikimu.

Kamishna Mkuu Msaidizi wa Ulinzi wa UNHCR Gillian Triggs akiwa Beni ameeleza kuwa kukosekana kwa amani, hatari zilizochanganyika zinazokabili watu waliohamishwa zitaendelea kuongezeka, na kusukuma familia katika hali ya kukata tamaa zaidi. “Lazima tuendelee kutetea haki za wanawake na wasichana ambao wanakabiliwa na hali hii mbaya, haswa kutokana na unyanyasaji wa kijinsia na ukatili.”

Goma

Wakiwa mjini Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, walishuhudia zaidi ya wakimbizi wa ndani 600,000 wakiwa wamejihifadhi katika majengo ya muda ambayo hayana vifaa vya kustahimili hali mbaya ya hewa.

Makamishna hao Wakuu wa UNHCR walishiriki katika ugawaji wa blanketi, turubai, na vitu vingine katika eneo la makazi la muda huko Luchagara, kilomita 13 tu kutoka Goma.

Mkuu Msaidizi wa Operesheni Raouf Mazou alisisitiza kuwa UNHCR itaendelea kuwasaidia “Tutaendelea kujitolea kutoa usaidizi wa kuokoa maisha na kuratibu huduma muhimu za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya kisaikolojia na utoaji wa makazi ya dharura.

Hata hivyo Mazou amesema jukumu hili ni la kila mtu “Idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na watu milioni 1.2 wamekimbia vita huko Kivu Kaskazini tangu Machi 2022, ni changamoto kubwa ambayo inahitaji msaada zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.”

Wajumbe wa ziara hiyo pia walisikia maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa familia kuhusu athari mbaya ya mzozo katika elimu ya watoto, na mwaka mzima wa masomo kupotea kwa sababu ya kuhama.

Biashara ya ngono

UNHCR na washirika wa misaada ya kibinadamu wameeleza pia kusikitishwa sana na ongezeko la unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana katika maeneo yenye msongamano wa watu kuyahama makazi yao.

Wameeleza wasiwasi mkubwa ni mwelekeo wa kuongezeka kwa ushiriki wa biashara ya ngono kutokana na uhaba wa chakula unaokabili kaya zilizohamishwa.

Wakati ukosefu wa usalama ukiendelea na mapigano makali yanaendelea kukumba eneo hilo, fursa kwa watu waliohamishwa kurejea makwao na maisha yao kwa usalama na utu bado ni finyu.

Rasilimali za ziada zinahitajika kwa haraka ili kuendelea kusaidia familia zilizohamishwa nchini DRC.

Kwa mwaka 2023, UNHCR hadi sasa imepokea asilimia 29 tu ya dola milioni 233 zinazohitajika kukidhi mahitaji ya watu waliokimbia makazi nchini humo.