Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia Namendea Lesiria amekamatwa na polisi akidaiwa kumpiga mkewe Mesoni Kashiro , mweye umri wa miaka 15, mkazi wa kijiji cha Gelailumbwa, Kata ya Gelailumbwa, Tarafa ya Ketumbeine, wilayani Longido Mkoa wa Arusha.
Mesoni inadaiwa alipigwa baada ya kufungwa kwenye mti, kisha kuchapwa fimbo na mume wake, Namendea Lesiria kwa kushirikiana na rafiki yake, ambaye jina halijafahamika kwa kosa la kumwaga dawa ya mbuzi.
Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani Longido, Atunagile Chisunga, watuhumiwa wapo kituo cha Polisi Longido na kesho Septemba 23,2022 watafikishwa mahakamani.
“Huu ni ukatili kabisa, kwanza ameolewa akiwa na umri mdogo, wamempiga wakiwa wamemfunga kamba na kumtundika kwenye miti,” alisema na kuongeza kuwa binti huyo aliyejeruhiwa yupo kituo cha afya Longido kwa matibabu.