Jamii imetakiwa kulipa umuhimu na kipaumbele suala la elimu kama nyenzo muhimu katika kuleta mabadiliko mbalimbali kwa jamii ikiwemo mabadiliko ya fikra, kuwa na fikra mbadala na hata kuwezesha jamii kubadilika.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Septemba 23, 2022 na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Hellen Kijo Bisimba akiwa katika mdahalo ulioandaliwa na Jukwaa la vijana la Reach out Tanzania ulioangazia mchango wa asasi za kiraia katika maendeleo nchini uliofanyika katika ukumbi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dkt. Kisimba amesema, asasi za kiraia zina mchango mkubwa katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na hata kuisaidia serikali katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi kwa kutekeleza majukumu ambayo pia yangeweza kufanywa na serikali.
Ameongeza kuwa, kuna wakati serikali haifikii malengo yake kutokana na sababu mbalimbali hivyo asasi za kiraia huisadia serikali kutimiza jukumu hilo.
“Kuna wakati serikali haifikii malengo yake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchache wa rasilimali, kufuatia hilo asasi za kiraia inakuja hapo kwa ajili ya kuziba hilo gap (uwazi) kati ya mahitaji ya raia na serikali inavyopaswa kukidhi mahitaji hayo” alisema Dkt. Kisimba na kuongeza
“Ingekuwa kwamba serikali inafanya kila kitu, hata asasi za kiraia zisingekuwepo, lakini jambo hilo haliwezekani ndio maana asasi za kiraia zipo dunia nzima”
Ameendelea kwa kusema kuwa, kuna asasi za kiraia ambazo zinafanya kazi ya kutoa huduma, ambazo zinaweza kufanywa na serikali, kuna ambazo zinajenga hospitali, vituo vya kulelea yatima, shule na vituo vya kutolea msaada wa kisheria zote hizi ni huduma za msingi na muhimu kwa wananchi.
Kando na hayo, Dkt. Kisimba amewakumbusha wananchi kufahamu umuhimu wa serikali na malengo yake pindi inapowekwa madarakani kwa kusema kuwa, baadhi ya malengo mahususi ni pamoja na kutatua changamoto za wananchi ikiwemo changamoto ya umasikini, kuwaletea maendeleo na kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa uhuru na furaha.