Bodi ya Parole yaridhia wafungwa 82 kuachiwa huru

Bodi ya Parole ya Taifa chini ya Mwenyekiti wake, Augustine Mrema imeridhia na kupitisha orodha ya wafungwa 82 kuachiwa huru kutoka gerezani. 

Kabla ya wafungwa hao kuachiwa huru majina yao yanapelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kujiridhisha na kuidhinisha waachiwe huru au la. 

Mrema alisema Dodoma jana kuwa bodi hiyo inayokutana mara nne kwa mwaka, imeridhia wafungwa 82 waachiwe isipokuwa watano ambao hawajafikia vigezo vya kuachiwa huru. 

Katibu wa kikao hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Mzee Ramadhani Nyamka alisema kikao hicho ni cha 46 tangu kuanza kwa mfumo wa Parole, kimeridhia wafungwa hao 82 kuachiwa huru au kutumia muda uliobaki wa kifungo chao kusaidia jamii. 

Nyamka alisema wanufaika na mfumo wa parole ni wale wafungwa wenye kifungo cha miaka minne hadi minane ambao wanakuwa wametenda makosa ya kawaida.