Bohari Kuu ya Dawa nchini Tanzania ilivyopiga fedha za Uviko-19

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini humo (PSPTB) kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika na ubadhirifu kwenye manunuzi ya vifaa vya afya katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambavyo vilipaswa kununuliwa kwa fedha za Uviko-19.

Majaliwa ameitaka Bodi hiyo kufika MSD Jumatatu Mei 9, 2022 kwa ajili ya kuanza kuwahoji waliohusika na ununuzi huo ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Majaliwa ametoa maagizo hayo katika uzinduzi wa wiki ya ununuzi wa umma uliofanyika jana ambapo uliratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na taasisi za ununuzi na ugavi ambazo ni PPRA,PPAA, PSPTF na GPSA jijini Arusha.

Amesema kuwa fedha hizo zilipaswa kununua vifaa hivyo ambavyo vingesambazwa katika hospitali za mikoa, wilaya zanahati na vituo vya afya kote nchini huku akionyesha namna ambavyo manunuzi yalivyofanya.

Amesema kuwa MSD walitakiwa kununua kipimo cha sukari ambacho kwa bei ya kawaida ni Sh150 ila wao wakanunua kwa Sh300, kipimo cha mkojo bei ya kawaida Sh200 kimoja wao wakanunua kwa zabuni Sh780, walikuwa wananunua kipimo kidogo cha hamolojia ya mwili kinauzwa Sh2, 100 wao wakununua kwa bei ya zabuni Sh4,500.

“Hawa walipaswa kununua kipimo kikubwa cha haimolojia ya mwili bei ya kawaida ni Sh3,800 wao wamenunua kwa Sh6,300 si mnaona bei e inavyokwenda karibu asilimia sijui 200,” amesema

“Walitakiwa kununua kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa figo kipimo muhimu sana na tungepata vingi tu, kinauzwa Sh6,000 wao wamenunua kwa Sh40,000.Walitakiwa kununua seti moja ya vitendanishi kwa ajili ya awamu moja ya kusafisha damu bei ya kawaida ambayo wangepaswa kununua ni Sh65,000 lakini wao wamenunua kwa Sh189,000,”amesema

Aidha  Waziri Mkuu amesema MSD walitakiwa wanunue mashine ndogo ya kipimo cha haimolojia ya mwili ambacho kinauzwa Sh5 milioni wao wamenunua kwa Sh14.045 milioni, huku wakitakiwa kununua mashine ndogo ya kupima kemia ya mwili ambayo bei ya kawaida ni Sh1.35 ila wao wamenunua kwa bei ya Sh6.7 milioni.

“Nyingine walitakiwa kununua mashine kubwa ya kupimia kemia ya mwili ambayo bei ya kawaida ni Sh10.5milioni wao wamenunua kwa Sh49 milioni. Hawa walitakiwa wanunue mashine ya kupima sukari kifaa hiki kinauzwa Sh7,956 wao wamenunua kwa Sh58,500,”

Ameongeza kuwa “Hawa walitakiwa kununua mashine kubwa ya kupimia haimolojia ya mwili hiki kifaa kinauzwa Sh20.8 milioni lakini Sh117 milioni, hawa pia walitakiwa wanunue kifaa kinaitwa mashine ya kupimia haimolojia ya mwili cha ukubwa kidogo bei ya kawaida ni Sh37.4 milioni wao wamenunua Sh149.4 milioni,”ameeleza

“Hawa walitakiwa kununua mashine ya kuchakata maji kwa ajili ya kutumika kusafisha damu kifaa kinauzwa Sh32.3 ila wao wamenunua kwa Sh129 milioni, hebu wataalamu wetu mtuambie ni kwa sababu ya nini, wataalamu wetu wa manunuzi kwa nini hili linatokea? kwa maslahi ya nani?“

“Huyu aliyeenda zoezi hili hakuzifata zingine PSPTB wanasema kazi yao ni kuangalia watu wanaofuatilia watu wenye taaluma hii wasipozingatia maadili,”

Kufuatia hayo Waziri Mkuu ameagiza wote waliohusika wanafatiliwa na siku ya Jumatatu Mei 9, atafika ofisi za MSD kwa ajili ya kupatiwa maelezo ya kina.

“Naanza na nyie hebu wafuatilinei hawa Jumatatu nawafwata huko MSD na wewe nikukute huko na umeshachukua hatua, Jumatatu nikukute pale wanipe maelezo  haya na mimi sitasita kwenda na Kamanda Sirro na Hamduni wa Takukuru ili washughulike na hao na tunapoanza na hao huwa hawabaki kazini,hii sio nia ya serikali kwenu nyie wataalam wetu,”amesema Waziri Majaliwa.